BENKI YA EQUITY TANZANIA YAZINDUA KAMPENI YA ‘KARIBU MEMBA’

Mkuu wa Kitengo cha Uendeshaji wa Benki ya Equity Tanzania Rojas Mdoe akizungumza katika hafla fupi ya uzinduzi wa kampeni ya ‘Karibu Memba’ jijini Dar es Salaam.

NA ABRAHAM NTAMBARA

BENKI ya Equity Tanzania imezindua kampeni ya ‘karibu memba’ yenye lengo la kuwashukuru wateja kwa kufanya nao huduma kwa miaka 10 toka ianze kutoa huduma nchini.

Akizungumza katika hafla fupi ya uzinduzi wa kampeni hiyo leo Juni 1, 2022 jijini Dar es Salaam Mkuu wa Kitengo cha Uendeshaji wa Benki hiyo Rojas Mdoe amesema wateja ni sehemu ya familia yao kwamba ndiyo maana wanawaita memba.

“Tumewahudumia kwa muda wote na kuwa vinara katika utoaji wa huduma kidigitali kama Dunia ya sasa inavyotaka, pia benki ipo mstari wa mbele kutoa huduma mbalimbali za kifedha ikiwa ni pamoja na, utunzaji fedha, Akaunti za watoto, vikundi, mikopo mbalimbali kama ya wakulima (kilimo biashara/Agribusiness), wastaafu, wafanyabiashara kubwa na ndogo ndogo, waajiriwa, watumishi wa umma na kadhalika,” amesema Mdoe na kuongeza kwamba,

“Akaunti zetu zote hazina makato ya kila mwezi na gharama za wakati wa kutoa au kutuma ni nafuu ukilinganisha na mabenki mengine,”.

Mdoe ameeleza kwamba ndani ya miaka 10, Benki ya Equity imeweza kutoa ajiri kwa Watanzania zaidi ya 430 na kubadilisha maisha ya Watanzania zaidi ya 500 kiuchumi na kijamii.

“Hivi karibuni tuliweza kuzindua mradi na taasisi mbalimbali kwa ajili ya mikopo ya wakulima tukiunga mkono Serikali katika kuhakikisha tunaipa nguvu sekta hii ya msingi katika ukuaji wa uchumi wa nchi yetu. Tuna makubaliano na taasisi mbalimbali kama Agricom na Yara ili kuhakikisha kuwa wakulima wanapata pembejeo kirahisi na kwa gharama nafuu,” ameongeza Mdoe.

Amebainisha kwa Benki hiyo imejikita katika kutatua changamoto za wananchi na itaendelea kutoa elimu na fursa mbalimbali zinazotolewa na benki kwa memba wa Tanzania na Dunia kwa ujumla.

Hivyo ametoa wito kwa wananchi wengine kujiunga na benki hiyo na kufurahia huduma zao mbalimbali kama za mikopo nafuu ili kuwafikia wafanyabiashara wadogo wadogo, wakulima wadogo na wakubwa, wakina mama na jamii nzima katika kuendelea kujikwamua kiuchumi.

Amesema kuwa Benki hiyo ni benki pekee yenye huduma nafuu na za kisasa/kidigitali kwamba hivi karibuni wamezindua kampeni yao mpya ya benki kidigitali inayoitwa ISHI KISASA-PESA MZIGO ikiwa na lengo la kusisitiza matumizi ya huduma za kibenki za kidigitali zinazoweza kumfanya mteja kupata huduma popote alipo bila hata kufika benki.

“Pia tunatoa elimu ya uwekezaji Amana, utunzaji fedha, pamoja na mikopo nafuu, hivyo hii ni fursa muhimu kwenu kwasababu mtapata uwezo wa huduma za kifedha, ushauri na elimu bora,” ameeleza Mdoe.

Post a Comment

0 Comments