Serikali Ichukue Hatua Uhaba wa Walimu Nchini


NA MWANDISHI WETU

Chama cha ACT Wazalendo kimeitaka Serikali kuchukua hatua  kuondosha changamoto sugu ya uhaba wa walimu kwenye shule shikizi nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo Ndugu Ado Shaibu kwenye Kata ya Mpepai Jimbo la Mbinga Mjini inayoongozwa na Diwani wa ACT Wazalendo Ndugu Donatus Donatus Mbepera.

Akiwa Katani hapo, Ndugu Ado Shaibu ametembelea na kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye Kata hiyo na kusikiliza changamoto zake.

Akikagua ujenzi wa madarasa katika shule Shikizi ya Mwamko, Ndugu Ado amempongeza Diwani Mbepera kwa kusimamia vizuri miradi ya elimu, afya na maji katika Kata yake. Hata hivyo, Katibu Mkuu alitoa rai kwa Serikali kuhakikisha Shule Shikizi zinapatiwa walimu zaidi ili kuwapunguzuia mzigo walimu wachache waliopo.

"Tumefarijika na jitihada zilizochukuliwa kwenye ujenzi wa madarasa. Lakini, bado kuna uhaba mkubwa wa walimu. Mathalani, hapa Shule Shikizi ya Mwamko, kuna Mwalimu mmoja tu anayefundisha Wanafunzi 187. Hili tunalichukua na tutalifikisha Serikalini"- alisema Ndugu Ado.

Akiwa katika Shule ya Sekondari ya Ali Mohamed Shein, Ndugu Ado alisema kuwa falsafa ya Chama cha ACT Wazalendo ni "Siasa ni Maendeleo" na Chama kinaitekeleza kwa vitendo.

"Mwaka 2018, Kiongozi wetu wa Chama Ndugu Zitto Kabwe alitembelea Kata zote zilizokuwa chini ya ACT Wazalendo. Chama kilichukua hatua, mbali na kuiwajibisha Serikali, kupunguza changamoto kwenye Sekta ya maji, afya, barabara na masoko. Leo tupo Mpepai. Tunawaahidi pia watu wa Mpepai kuwa changamoto zote tumezichukua na tutawashirikisha wadau kuzitatua"-Aliongeza Ndugu Ado.

Ndugu Ado anaendelea na ziara kwenye Majimbo yote ya Mkoa wa Ruvuma ambapo leo atafanya vikao katika Majimbo ya Mbinga Mjini na Nyasa.

Janeth Rithe, 
Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma, 
ACT Wazalendo, 
13 Juni 2022.

Post a Comment

0 Comments