SUSAN BUFFET FOUNDATION KUIPATIA TANZANIA DOLA MILIONI 15 KWA AJILI YA HUDUMA ZA AFYA YA UZAZI

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu akiwa na Mtendaji Mkuu wa STBF Prof. Senait Fisseha mara baada ya mazungumko yao ambapo  Taasisi hiyo imeahidi kuipatia tanzania Dola Milioni 15 kwa ajili ya huduma  ya afya ya Uzazi, mama na mtoto.

Waziri wa Aya Ummy Mwalimu akiwa  kwenye picha ya pamoja na Mtendaji Mkuu wa STBF Prof. Senait Fisseha. Kulia baada ya waziri ni Mkurugenzi Msaidizi kitengo cha Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto Dkt. Ahmad Makuwani na mwisho kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Idara ya kinga Dkt. Beatrice Mutayoba 
Kutoka Paris,Ufaransa

Taasisi ya Suzan Thompson Buffet Foundation (STBF) yenye Makao Makuu yake nchini Marekani imekubali kutoa msaada wa dola za Kimarekeni milioni 15 sawa na shilingi za Kitanzania bilioni 34.5 kwa ajili ya kuimarisha utoaji wa huduma za afya ya Uzazi ,Mama na Mtoto kwa kipindi cha miaka mitatu.

Hayo yamebainishwa  katika mazungumzo yao baina ya Waziri wa Afya, Mhe Ummy Mwalimu na Mtendaji wa taasisi hiyo Prof. Senait Fisseha katika kikao cha 14 cha Wafadhili wa Afya ya Mama, Mtoto na Vijana (Global Financing Facility for Women Children and Adolescent Health) Jijini Paris.

Waziri Ummy amesema fedha hizo zitasaidia kuimarisha utoaji wa huduma za afya ya uzazi ikiwemo kuhakikisha kuwa watoa huduma wa afya ngazi ya msingi ya jamii wanapatikana wa kutosha.

Aidha, Waziri Ummy amemshukuru Prof. Senait na kuahidi kuwa fedha hizo zitasimamiwa kikamilifu ili kuleta matokeo yaliyokusudiwa  ya kuokoa maisha ya wanawake, watoto na vijana.

Ameongeza kuwa fedha hizo zitaelekezwa kuimarisha utoaji wa huduma kwenye vituo vya kutolea huduma ikiwemo huduma rafiki kwa vijana.

Naye, Prof. Senait amesema ameiona dhamira  njema ya Rais wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha huduma za afya ya Uzazi, Mama na Mtoto hivyo wapo tayari kumuunga mkono ili aweze kutimiza vyema maono yake

Hivyo Taasisi ya STBF imeonesha nia ya kuongeza fedha zaidi kwa Tanzania endapo utekelezaji wa msaada huo utakuwa wa mafanikio.

Post a Comment

0 Comments