WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima.
NA ABRAHAM NTAMBARA
WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima ameitaka Jamii kuendelea kupaza sauti kupinga vitendo vyote vya ukatali na vinavyoashiria ukatili kwa Jamii hususan kwa wazee.
Kauli hiyo ameitoa leo Juni 10, 2022 jijini Dar es Salaam akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Maadhimisho ya siku ya kupinga ukatili dhidi ya wazee duniani Juni 15, 2022.
“Pia natoa wito kwa jamii kutoa taarifa za viashiria vya ukatili au ukatili katika vyombo husika vipivyo karibu na jamii na kama ikishindikana basi piga namba 116 bila malipo masaa 24 kila Siku piga,” amesema Waziri Gwajima na kuongeza kwamba,
“Pia piga au tuma ujumbe kwenye simu za maafisa ustawi na maendeleo ya Jamii wa Wizara waliopo kila Mkoa na maafisa wa Wizara za Kisekta ikiwemo namba ya Waziri mwenye dhamana 0734134191,”.
Akizungumzia kuhusu Maadhimisho hayo, Waziri Gwajima ameeleza kwamba Siku hii huadhimishwa kufuatia azimio la umoja wa mataifa Na. 66/127 la Desemba 2011 lililotokana na maombi ya Shirika la Mtandao wa Kimataifa wa kuzuia ukatili dhidi ya wazee.
Kwamba azimio hilo liliamua kuwa na Siku moja kwa mwaka kwa ajili ya kupaza sauti ili kupinga vitendo vya ukatili dhidi ya wazee ikiwemo ukatili wa kimwili, kihisia na kiuchumi.
“Kila mwaka Maadhimisho haya hubeba kauli mbiu yenye ujumbe mahususi kuhusiana na wazee. Kwa mwaka huu 2022, kauli mbiu inasema 'Tuhakikishe wazee wanalindwa, wanasikilizwa na kuheshimiwa, tusikose kuhesabiwa kwenye Sensa ya Watu na Makazi,” amesema Dkt. Gwajima.
Waziri Gwajima amebainisha kwamba kauli mbiu hiyo inatoa wito kwa jamii yetu kuhakikisha wazee wanalindwa, wanasikilizwa na kuheshimiwa katika nyanja zote.
Vile vile amesema inasisitiza ushiriki wa Makundi yote ikiwemo wazee katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi Agosti 23 mwaka huu kwani takwimu za Sensa zitasaidia Serikali katika mipango ya huduma na maendeleo kwa wananchi wake wakiwemo wazee.
Aidha Waziri Gwajima amesema Maadhimisho haya kwa mwaka huu yataadhimishwa katika ngazi ya mikoa ambapo Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum itashiriki katika Mkoa wa Singida.
Kwamba lengo la Maadhimisho haya ni kuelimisha jamii kuhusu kupinga ukatili wa aina zote dhidi ya Wazee ambao ni ukatili wa kimwili, kihisia na kiuchumi.
Pia, Maadhimisho ya mwaka huu yanalenga kuelimisha jamii juu ya changamoto mbalimbali zinazowakabili wazee zinazotokana na mila na desturi potofu, fursa walizonazo na masuala ya uzee na kuzeeka.
Hivyo amesisitiza kila Mkoa kufanya Maadhimisho hayo, ya kupinga ukatili kwa wazee ili kujenga uelewa katika jamii kuhusiana na masuala ya ukatili hususan ukatili kwa wazee.
0 Comments