UVUNJWAJI WA SOKO LA MANZESE B HALMASHAURI YA MANISPAA YA SONGEA USITISHWE.



NA MWANDISHI WETU

Chama cha ACT Wazalendo kimeitaka Serikali kusitisha mpango wa kuvunja Soko la Manzese B lililopo Manispaa ya Songea hadi wafanyabiashara wa soko hilo wataposhirikishwa vya kutosha na kulipwa fidia.

Rai hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo alipokwenda sokoni hapo jana tarehe 16 Juni, 2022 na kufanya Kikao na wafanyabiashara wa soko hilo.

"Nimeambiwa Serikali inataka kuvunja soko hili na kujenga soko jipya la Kisasa. Hatua hiyo ni njema. Lakini ninafahamu soko hili lilijengwa na nyinyi wafanyabiashara na Mkataba wenu na Halmashauri unamalizika Mwaka 2025. Hivyo basi si haki kwa Serikali kutaka kulivunja kabla ya kuzungumza na nyinyi na kuwalipa fidia"-Alisema Ndugu Ado.

"Nimeelezwa kuwa mmepewa notisi ya kuhama ifikapo tarehe 1 Julai, 2022. Ninamuomba Waziri Mwenye dhamana ya TAMISEMI Ndugu Innocent Bashungwa kuingilia suala hili. Mradi huu hauwezi kutekelezwa kabla ya kuwalipa fidia wafanyabiashara na kuwatafutia maeneo mazuri ya kwenda. Pia, mradi ukikamilika, wafanyabiashara wa sasa wapewe kipaumbele kupewa maeneo"-Aliongezea Ndugu Ado.

Ndugu Ado alitoa wito pia kwa Mh. Rais Samia Suluhu Hassan kuwamulika Wawakilishi wake wa ngazi za chini kwa sababu baadhi ya maamuzi yao yanawaumiza Wananchi masikini na hivyo kuipaka matope Serikali.

"Soko hili lina wafanyabiashara 700. Unapowaumiza watu 700 unakuwa umeumiza maelfu ya familia zao na kuwajengea chuki na Serikali"-Alisisitiza Ndugu Ado.

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kuhakikisha Serikali za Vijiji zinazingatia taratibu za uuzaji wa ardhi ya kijiji.

Ndugu Ado alitoa rai hiyo alipotembelea Kijiji cha Kipingo kilichopo Jimbo la Madaba mapema jana tarehe 16 Juni 2022. Wananchi wa Kijiji hicho walimlalamikia Ndugu Ado juu ya kitendo cha Serikali ya Kijiji kuuza zaidi ya hekari 1500 za Kijiji bila baraka za Mkutano Mkuu wa Kijiji. Wanakijiji hao wanadai wale ambao wamekuwa wakihoji dhidi ya suala hilo wamekamatwa na Polisi, kupigwa na kubambikiwa kesi.

Ndugu Ado aliwaahidi Wanakijiji hao kuwa Chama cha ACT Wazalendo kupitia Kamati ya Kuisimamia Serikali ya Wasemaji wa Kisekta watalifuatilia suala hilo.

Imetolewa na:

Janeth Joel Rithe, 
Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma, 
ACT Wazalendo.
17 Juni 2022.


Post a Comment

0 Comments