WAZIRI MKUU AMWAHIDI RAIS SAMIA UTUMISHI ULIOTUKUKA


Na MWANDISHI WETU, Nachingwea


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemhakikishia Rais Samia Suluhu Hassan kuwa atatumia akili, nguvu na  uwezo wake wote kumsaidia ili kuhakikisha anafanikisha malengo yake ya kuwatumikia Watanzania.

Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema hayo katika mkutano wa majumuisho ya Ziara ya Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa NEC ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, aliyekuwa Mkoa wa Lindi kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM na Uhai wa Chama.

"Naomba nitamke hili mbele ya wana Lindi wenzangu, tangu Rais Samia ameingia madarakani na kuridhia mimi kuendelea na nafasi hii sijawahi kutamka, nataka kumshukuru yeye kwa kutuamini wana lindi.

"Nawashukuru wana Lindi kwa uvumilivu wenu maana kuna wakati huwa sipatikani, lakini naomba niwaahidi nitaendelea kufanya kazi kwa karibu na Rais Samia...namuahidi Rais Samia nitamsaidia kwa nguvu zangu zote, uwezo wangu wote kuhakikisha tunafanikisha malengo yake, wana Lindi tuendelea kumuunga mkono Rais na kila anachofikiria basi tuwe wa kwanza kumsaidia," amesema.

Waziri Mkuu amesema Mkoa wa Lindi sasa una mabadiliko kutokana na jitihada zinazofanywa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia serikali inayoongozwa na Rais Samia. 

"Wana Lindi nataka kuwaambia fursa ambayo tumeipata wana lindi ya kuheshimiwa ya kupata mtumishi wa kumsaidia kazi mheshimwa Rais kutoka miongoni mwetu wana Lindi, na mimi namjua vizuri kwa umahiri wake, uwezo wake na hata anapotoa maelekezo mkoa wa Lindi nao umekuwa ukiguswa," amesema.

Amesema kazi kubwa iliyopo ni kuhakikisha Ilani ya Uchaguzi ya CCM inayosimamiwa na Rais Samia, sisi tuwe watu wa kwanza kutekeleza, "jukumu letu ni kumsemea, jukumu letu kumuunga mkono, wote ambao tuko hapa tufahamu Rais Samia  ndio kiongozi wetu, tutaendelea kumuunga mkono kwa kila hatua."

 
MAELEKEZO YA CHAMA

Akizungumza kuhusu maagizo ya Shaka ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, Majaliwa alisema wameyapokea yote na kuahidi kuyafanyia kazi, na kuagiza kila mmoja kwenye wilaya yake ahakikishe anatimiza wajibu wake.

Alisema kuhusu Barabara Masasi , Nachingwea hadi Liwale kujengwa kwa kiwango cha lami, alisema imeshaingia kwenye mpango wa utafutaji fedha.

"Umezungumzia wanyamapori nami nimepokea, mbunge wa Nachingwea alikuja bungeni mezani kwangu kunieleza, nilimuagiza waziri wa maliasili apite huku Liwale Nachingwea, Lindi Vijiji hadi maeneo ya Milola, Naibu Waziri alikuja, amepita ameona," amesema.

ALICHOSEMA SHAKA

Kwa upande wake Shaka amesema, amezunguka katika Mkoa huo na kushuhudia kazi nzuri ya kuwahudumia wananchi kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

"Kwenye elimu tumetembelea shule ya wasichana jimbo la Mchinga, tumeshiriki ujenzi na tumeona utayari wa serikali katika kuboresha sekta ya elimu, Rais Samia amekuwa kinara wa kuwajengea uwezo watoto wa kike ili kuwa na taifa lenye wanawake wenye uwezo wa kulitumikia taifa," aliema.

Post a Comment

0 Comments