ADO SHAIBU: HATUA ZA DHARURA ZICHUKULIWE KUWANUSURU WANANCHI WA KIGAMBONI


NA MWANDISHI WETU

Chama cha ACT Wazalendo kimeitaka Serikali kuchukua hatua za dharura kuwanusuru Wananchi wa Kigamboni dhidi ya adha ya usafiri wa Kigambani kuelekea maeneo mengine ya Dar es salaam.

Rai hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo Ndugu Ado Shaibu kwenye Mkutano Mkuu wa ACT Wazalendo Jimbo la Kigamboni uliofanyika leo tarehe 01 Juni 2022 katika Kata ya Kigamboni.

"Ili Mwananchi wa Kigamboni aweze kwenda mjini, ni lazima apitie Daraja la Kigamboni au Kivukoni. Kwa upande wa darajani, ni lazima kulipia magari. ACT Wazalendo tunajua daraja hili lilijengwa kwa ubia na NSSF. Hoja yetu ni kuwa tozo ya kuvuka darajani iondoshwe. Kilichokusanywa kinatosha. Sehemu ya mkopo iliyobaki ilipwe na Serikali. Hatua ya Serikali ya hivi karibuni ya kupunguza tozo haitoshi, tozo zifutwe kabisa" alisema Ndugu Ado Shaibu.

Kuhusu Kivuko, Ndugu Ado alisema ni dhahiri kuwa Mamlaka ya Vivuko Nchini (TAMESA) imeshindwa kuendesha vivuko vya Kigamboni kwa sababu hakuna ukarabati wa vivuko wa mara kwa mara na Wananchi wanalazimika kutumia muda mwingi kwa sababu vivuko vya Mv. Magogoni, Mv. Kigamboni na Mv. Kazi kuharibika mara kwa mara.

"TAMESA iwajibike juu ya hili. Hata CAG ametaja ubadhirifu mkumbwa wa zaidi ya Milioni 410 kwenye  mafuta ya vivuko pekee. Ni lazima Menejimenti ya vivuko iwajibishwe au viwekwe chini ya Msimamizi mwingine"-Alisisitiza Ndugu Ado.

Ndugu Ado amesema kuwa ACT Wazalendo kupitia Kamati ya Wasemaji wa Kisekta ya Chama itaendelea kupaza sauti dhidi ya madhila na changamoto zinazowakabili Wanakigamboni na Watanzania kwa ujumla.


Imetolewa na:


Janeth Joel Rithe,
Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma,
ACT Wazalendo,
01 Juni, 2022.

Post a Comment

0 Comments