IET KUFANYA KONGAMANO LA 32 LA KITAIFA JIJINI ARUSHA, WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA MGENI RASMI




Rais wa Taasisi ya Wahandisi Tanzania (IET) Mhandisi Dkt. Gemma Modu akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

NA MWANDISHI WETU

TAASISI ya Wahandisi Tanzania (IET) inatarajia kufanya Kongamano la 32 la Kitaifa (National Conference) Novemba 30 hadi Desemba 2 Mwaka huu katika Ukumbi wa Kimataifa Arusha (AICC), jijini Arusha.

Hayo yamebainishwa leo Novemba 23, 2023 na Rais wa IET Mhandisi Dkt. Gemma Modu akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Mhandisi Dkt. Modu amesema Kongamano hilo wanaliandaa kwa kushirikiana na Bodi ya Usaili wa Wahandisi (ERB) na Chama cha Wahandisi Washauri Tanzania (ACET).

“Tunatazamia Wahandisi, mafundi wanafunzi na wadau wengine kutoka mikoa mbalimbali nchini na nje ya nchi watashiriki Kongamano hili muhimu na kuna baadhi ambao watashiriki kwa njia ya mtandao. Tunakadiria kuwa na washiriki zaidi ya elfu moja (1000),” amesema Mhandisi Dkt. Modu.

Kwamba katika Kongamano hilo mgeni rasmi atakuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa.

Amesema dhima ya mkutano huo ni “Innovative Solutions in Engineering for Sustainable Development” ambapo kwa tafsiri ni “Suluhisho za Ubunifu katika Uhandisi kwa Maendeleo Endelevu).

Mhandisi Dkt. Modu ameeleza kuwa dhima hiyo na kwa kuzingatia kwamba leo Dunia ipo kwenye zama za utandawazi wa Karne ya 21.

“Na tunaishi kwenye uchumi na jamii, zinazoendeshwa kwa nguvu ya Teknolojia ambayo maendeleo yake ni makubwa na ya Kasi na yanayochochewa zaidi na Mapinduzi ya kidigitali na unaandamana na Ubunifu wa kisayansi na matumizi yake ni ya lazima ili kuleta tija katika uzalishaji wa bidhaa, Utoaji huduma na uendeshaji wa Mifumo,” ameongeza Mhandisi Dkt. Modu na kueeleza,

“Kwa kuzingatia hayo, tunapaswa kufahamu kuwa, utekelezaji wa mikakati mbalimbali ya Maendeleo unahitaji sio tu Kukuza ujuzi na maarifa katika Uhandisi bali pia Kukuza kiwango na uwezo wa Ubunifu wa kisayansi na Teknolojia na ujuzi nyingine muhimu za Karne ya 21 zikiwemo nidhamu, umakini, ufanisi, uwezo, juhudi, weledi, uwajibikaji na kadhalika,” ameeleza Mhandisi Dkt. Modu.

Mhandisi Dkt. Modu ameeleza kuwa lengo ni ili kuweza kuendana na kukidhi matakwa ya Maendeleo ya Teknolojia na kuweza kusaidia Nchi kutatua changamoto katika Sekta mbalimbali za kiuchumi, pia kutoa suluhusho la matatizo katika jamii.

Ametumia fursa hiyo kuwakaribisha Wahandisi na wadau wote wa Sekta mbalimbali za uchumi nchini kushiriki kwenye Kongamano hilo muhimu.

Amewakumbusha Wahandisi na mafundi ambao bado hawajajiunga na Taasisi ya Wahandisi wajounge.

Kwa upande wake Mjumbe wa Baraza la Utendaji wa IET Mhandisi Pendo Haule akizungumza kuhusu ushiriki wa Wahandisi wazawa kwenye Miradi ya Serikali, amesema wamekuwa wakishiriki.

Kwamba Serikali imekuwa ikiwashirikisha kama Kampuni  moja moja ama kwa Wahandisi kuungana na kuchukua tenda.

Mfano wa miradi ambayo Wahandisi wazawa wameshirikishwa ni katika ujenzi wa Mradi wa miundombinu ya Mawasiliano.

Hivyo ameomba na kuhimiza makampuni ya wazawa kujitokeza kuchukua Miradi pindi inapotangazwa ili kuonesha ujuzi na utaalam wao.

 

 

 

Post a Comment

0 Comments