BODI ZA PURA NA ZPRA ZAKUTANA KUJADILI NAMNA YA KUTANGAZA VITALU KUVUTIA WAWEKEZAJI SEKTA YA MAFUTA NA GESI

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) Halfan Halfan akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) Mhandisi Charles Sangweni akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Taasisi ya Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia Zanziber (ZPRA) Ali Mirza akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mwendeshaji wa ZPRA Adam Abdulla Makame akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

NA ABRAHAM NTAMBARA

BODI za Wakurugenzi za Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) na Taasisi ya Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia Zanziber (ZPRA) zimekutana kujadili namna ya kutangaza vitalu ili kuvutia wawekezaji katika Sekta ya Mafuta na Gesi.

Akizungumza na Waandishi wa habari leo Disemba 4, 2023 Jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya PURA Halfan Halfan amesema wamekutana kwa mara ya kwanza tangu Mamlaka hizo mbili ziliposaini makubaliano (MoU) ya ushirikiano Mwaka jana.

“Madhumuni ya kukutana leo, kwanza tunajenga nyumba moja Tanzania, hivyo ni muhimu tukutane, tubadilishane mawazo namna ya kuendeleza Sekta hii ya Mafuta na Gesi nchini,” amesema Halfan na kuongeza,

“Matokeo ya mkutano huu tutazidisha ushirikiano zaidi katika kuendeleza Sekta hii, hivyo PURA kwa Bara na ZPRA kwa Zanziber tunataka kufanya kwa pamoja zoezi la kunadi maeneo yaliyowazi kwa ajili ya Uwekezaji na kuzishauri Serikali kutekeleza Sera ili kuhakikisha tunapata wawekezaji kwenye Sekta hii,”.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa PURA Mhandisi Charles Sangweni amesema kwamba kama Watendaji wa PURA na ZPRA wamekuwa na mashirikiano ya muda mrefu.

“Lakini tumezidisha mashirikiano baada ya kusaini makubaliano (MoU), hivyo tukaunda timu ya pamoja,” amesema Mhandisi Sangweni.

Mhandisi Sangweni ameeleza kuwa wamekuwa wakishirikiana katika kubadilishana uwezo na wamekuwa wakibadilishana taarifa mbalimbali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na kujengeana uwezo.

“Hivyo tukaona sio vyema kufanya mambo yetu bila kushirikisha Bodi zetu, hivyo mipango yetu ni kunadi vitalu ambavyo vitawekezwa,” amesema Mhandisi Sangweni na kuongeza,

“Hivyo tumeona ni vyema kushirikiana kuleta manufaa ya pamoja, pamoja na mambo mengine tutakubaliana namna ya kwenda kunadi vitalu kwa pamoja,”.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya ZPRA Ali Mirza amebainisha kuwa Mwaka jana PURA na ZPRA zilisaini makubaliano (MoU) namna ya kushirikiana katika Sekta ya Mafuta na Gesi.

Hivyo ameeleza kuwa mkutano huo utakuja na maazimio Maalum ambayo watayaadili namna ya kwenda kuyatekeleza kwa maslahi mapana ya pande zote mbili.

Kadhalika Mkurugenzi Mwendeshaji wa ZPRA Adam Abdulla Makame amesema kwamba wamekutana ikiwa ni kikao cha kwanza cha Bodi zote mbili kwa lengo la kujadili ushirikiano wa kuendeleza Sekta ya Mafuta na Gesi.

“Hivyo tunategemea Kufikia makubaliano ya Pamoja, na kujua tutatangaza vipi vitalu vyetu kwa ajili ya kuvutia wawekezaji,” amesema Makame.

Post a Comment

0 Comments