NA MWANDISHI WETU
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewasisitiza waumini wa Dini ya Kiislamu na wananchi kwa ujumla kuhurumiana na kuwasaidia wasio na uwezo, hususan katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
Rais Dkt. Mwinyi ametoa wito huo leo, tarehe 20 Februari 2026, alipojumuika na waumini katika Sala ya Ijumaa iliyosaliwa Msikiti wa Al Abrar, Fuoni Chunga, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amewakumbusha wafanyabiashara kutopandisha bei za bidhaa za chakula ili kuwawezesha wananchi kumudu mahitaji ya futari.
Halikadhalika, amewataka wakaazi wa Fuoni Chunga kutoyauza maeneo yao kufuatia kupanda kwa thamani baada ya ujenzi wa barabara, na kusisitiza umuhimu wa kulinda maeneo ya kilimo kwa ajili ya uzalishaji wa chakula na matunda.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Afisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Khalid Ali Mfaume, amewahimiza waumini kumcha Mwenyezi Mungu na kuzingatia matendo ya halali.
Rais Dkt. Mwinyi ameendeleza utaratibu wake wa kushiriki Sala ya Ijumaa katika misikiti mbalimbali mjini na vijijini.
0 Comments