KAMATI YA USHAURI LONGIDO YAPENDEKEZA SOKO NA STENDI KUPEWA KIPAUMBELE BAJETI YA 2026/2027







NA MWANDISHI WETU, LONGIDO

Kamati ya Ushauri Wilaya ya Longido imeshauri ujenzi wa Soko la Kisasa na Stendi ya Kisasa kuwa miongoni mwa vipaumbele muhimu katika Bajeti ya Halmashauri kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027.

Ushauri huo umetolewa leo Februari 20, 2026, wakati wa kikao maalum cha Kamati hiyo kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri J.K. Nyerere, kwa lengo la kupitia na kutoa ushauri kuhusu mapendekezo ya Mpango na Bajeti ya Halmashauri kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 yenye makisio ya jumla ya shilingi bilioni 41,287,492,000.00 kwa ajili ya matumizi ya kawaida (OC), mishahara (PE) na miradi ya maendeleo.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Longido, Mhe. Salum Kalli, amesema kuwa ujenzi wa soko na stendi utachochea mzunguko wa fedha, kuongeza mapato ya Halmashauri na kuharakisha ukuaji wa Wilaya hiyo kwa kuvutia wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi.

“Twendeni tukafanye kazi na kusimamia haya vizuri. Ujenzi wa soko la kisasa na stendi ya kisasa hapa Longido ni jambo muhimu sana. Watu wanataka mzunguko wa pesa kwani utavutia wafanyabiashara wa nchi jirani kama Kenya kuja kufanya biashara hapa,” amesema Mhe. Kalli.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Longido, Papa Nakuta, amesema tangu kuanzishwa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Longido mwaka 2007, wilaya hiyo imekuwa ikikosa kasi ya ukuaji kutokana na kutokuwa na soko na stendi za kisasa, miundombinu ambayo ingeweza kuichangamsha kiuchumi.

“Kungekuwa na soko la kisasa na stendi ya kisasa, na kufanya kazi kwa saa 24, Longido ingeongeza mapato ya Halmashauri na watu wangevutika kujenga hapa,” amesema Mhe. Nakuta.

Amesisitiza kuwa ujenzi wa miundombinu hiyo ni wa muhimu na wenye tija kwa Wilaya, kwani utawavutia wafanyabiashara kujenga fremu za biashara na kuongeza mapato ya Halmashauri pamoja na kuinua kipato cha wananchi kupitia ongezeko la mzunguko wa fedha.

Akizungumzia mapendekezo ya bajeti, ameshauri miradi viporo ikamilishwe kwanza kabla ya kuanza utekelezaji wa miradi mipya ili kuhakikisha ufanisi na tija katika matumizi ya fedha.

Naye Katibu wa CCM Wilaya, Ndugu Geodfrey Kavenga, amepongeza bajeti iliyopendekezwa akisema imegusa sekta mbalimbali muhimu, huku akiomba kuwepo kwa usimamizi madhubuti wakati wa utekelezaji ili fedha zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Longido, Steven Kiruswa, amepongeza rasimu ya bajeti hiyo na kupendekeza Halmashauri itafute mikopo kutoka kwa wadau wa maendeleo ili kuharakisha utekelezaji wa miradi, akieleza kuwa Halmashauri ina uwezo wa kukopesheka.


Post a Comment

0 Comments