KAMPUNI ya Mahindra kutoka India kwa ubia na Kampuni ya GF Truck
wanatarajia kuanza uzalishaji na uuzaji wa magari hapa nchini.
Hayo yamebainishwa leo Desemba 5, 2023 na Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo katika hafla ya uzinduzi
wa uwepo Kampuni ya Mahindra nchini sambamba na uzinduzi wa magari yaliyozalishwa
na Kampuni hiyo kwa ushirikiano na GF Truck.
Prof. Mkumbo ameeleza kuwa uzalishaji wa magari hayo nchini unatarajia
kuanza miezi sita ijayo kuanzia hivi sasa.
Hivyo Waziri Prof. Mkumbo amesema kutokana na Kampuni kuzalisha
magari nchini, Serikali ina mpango wa kuifanyia marekebisho sheria ya uagizaji
magari nchini ambayo inaruhusu hadi magari chakavu kuingia nchini ili kuzuia magari
hayo na kulinda maslahi ya Viwanda vya uzalishaji wa magari nchini.
Waziri Prof. Mkumbo amesisitiza kwa kusema kwamba, kwa sasa hapa nchini kumekuwa na viwanda
vinavyotengeneza magari hivyo ni wakati wa kubadilisha sheria ya uigizaji
magari.
"Sheria ya sasa inaruhusu mpaka magari chakavu yaingie
nchini hivyo sheria tutaibadilishe ili kulinda viwanda hivi vinavyozalisha
magari hapa nchini,” amesema Prof. Mkumbo.
Hata hivyo, Prof. Mkumbo amesema ujio wa kampuni ya Mahindra
ni matokeo ya ziara ya Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania aliyoifanya
nchini India mwezi Oktoba mwaka huu ambapo alikutana na kuzungumza na wawekezaji
mbalimbali.
"Haya ni matunda ya ziara ya Rais Samia nchini India
imepelekea ujio wa Kampuni hii kikubwa kuja kuwekeza hapa nchini,” ameongeza l.
Kwa Upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania
(TIC), Gilead Teri, amesema kwa sasa hali ya uwekezaji Tanzania ni nzuri huku
akiwataka Watanzania kujitokeza kwenye uwekezaji kwa kushirikiana wa wageni
kutoka nje.
"Kama wewe Mtanzania unakiwanja, nyumba, shule, kiwanda
na unataka ubia na mwekezaji njoo kwetu sisi tutakutafutia uwekezaji na mbia,” amesema
Teri.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa GF Group, Iman Karmali, amesema
wapo nchini kwa miaka 17 na wameweza na kutoa ajira za moja kwa moja kwa
Watanzania zaidi ya 250 na kubainisha kuwa GF Group na Mahindra mwakani
wataanza kuzarisha magari madogo.




0 Comments