Na Lydia Lugakila, Bukoba
Kufatia kuwepo kwa mahitaji makubwa ya uwanja mkubwa wa Ndege, Mkuu wa Mkoa wa Kagera Hajjat Fatma Mwassa amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ameridhia kutoa fedha za ujenzi wa uwanja mpya wa Ndege katika maeneo ya Kyabajwa wilayani Missenyi.
Akitoa taarifa hiyo kwenye kikao cha bodi ya Barabara kilichofanyika katika ukumbi wa Mkoa huo Mwassa amesema kuwa ujenzi wa uwanja huo umezingatia mahitaji makubwa ya usafiri wa anga ambao umekuwa ni maisha ya watu wa Kagera sambamba na urahisishaji wa usafirishaji wa mizigo mikubwa tofauti na sasa ambapo ndege kubwa haziwezi kutua
Aidha amewaomba Wananchi Mkoani Kagera kutoanzisha mivutano na migogoro yenye lengo la kukwamisha mradi huo sambamba na kueleza kuwa mradi wa ukarabati wa bandari za Kemondo na Bukoba umefikia hatua nzuri na sasa Meli kubwa zitaana kutia nanga.
Kwa upande wake mbunge wa Jimbo la Bukoba Vijijini Dkt. Jasson Rweikiza ameishukuru serikali kwa ujenzi wa uwanja huo ambao unakwenda kufungua fursa nyingi za kibiashara na kiuchumi kwa wananchi wa Kagera.
Ameongeza kuwa ujenzi wa uwanja huo uende sambamba na ujenzi wa Daraja la Kansinda ambalo litarahisisha mawasiliano kwa wananchi kwakuwa ni maeneo ambayo yapo karibu na eneo unapokwenda kujengwa uwanja wa Ndege.

0 Comments