NAIBU WAZIRI APONGEZA MAKUMBUSHO YA TAIFA KWA MIKAKATI YA KUKUZA UTALII WA URITHI NCHINI.





​DAR ES SALAAM: Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), amepongeza jitihada na mikakati inayotekelezwa na Makumbusho ya Taifa la Tanzania katika kuhifadhi, kuendeleza, na kutangaza urithi wa kihistoria na malikale nchini.

​Mhe. Chande ametoa pongezi hizo leo, Julai 15, 2026, alipotembelea Makao Makuu ya Makumbusho ya Taifa na Kijiji cha Makumbusho jijini Dar es Salaam. Ziara hiyo ilikuwa na lengo la kukagua maeneo hayo ya urithi, kujionea maendeleo yake, pamoja na kuhamasisha uboreshaji wa vivutio vya utalii kuelekea  Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027).

​"Jitihada hizi za Makumbusho ya Taifa zina mchango mkubwa sana katika kukuza utalii wa urithi nchini na kuongeza thamani ya vivutio vyetu," alisema Mhe. Chande.
Katika ziara hiyo, Naibu Waziri alipokelewa na Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dkt. Noel Biseko Lwoga, ambaye aliwasilisha mikakati mbalimbali inayotekelezwa na taasisi hiyo ambayo ni pamoja na ​uboreshaji wa miundombinu na maonesho ya makumbusho kidigitali,
​Uimarishaji wa uhifadhi wa urithi wa taifa.

​Pia alisisitiza mipango ya uboreshaji wa huduma ili kuongeza uzoefu wa kipekee kwa wageni wakati wa AFCON 2027.

​Wakati wa ziara hiyo, Mhe. Chande alitembelea maonesho mbalimbali na kujionea maonesho mbalimbali ikiwemo nyumba za asili za makabila ya Tanzania zilizopo Kijiji cha Makumbusho, ambapo alipata taarifa za kina  kuhusu historia, mila, na desturi zinazounda utambulisho wa Taifa la Tanzania.

​Akihitimisha ziara yake, Mhe. Chande ameitaka Menejimenti ya Makumbusho ya Taifa kuendeleza kasi ya utekelezaji wa mikakati hiyo ili kuhakikisha maeneo hayo yanazidi kuwa vivutio vikuu vya utalii, yanaleta wageni wengi zaidi, na kuchangia kwa kasi ukuaji wa uchumi kupitia sekta ya  Makumbusho na Malikale.

Post a Comment

0 Comments