Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro inaendelea kuvitangaza vivutio vya utalii vilivyopo ndani na nje ya Ngorongoro ili kuidhihirishia dunia kuwa eneo hilo ni hazina ya ulimwengu.
Akitoa maelezo kwa kaimu mkurugenzi wa idara ya Afrika kutoka wizara ya mambo ya nje ya Sweden bwana Dario Jovic, Afisa Mhifadhi mkuu wa Ngorongoro anayeshughulikia Masoko bwana Michael Makombe amesema pamoja na kreta ya Ngorongoro hifadhi hiyo ina mapango ya tembo na maporomoko ya maji ambayo mtalii akifika katika eneo hilo huondoa msongo wa mawazo.
Amevitaja vivutio vingine kuwa ni pamoja na kreta za Empakai na Olmoti,mchanga unaohama, mlima Lolmalsin, tambarare za mazalia ya Nyumbu Ndutu, mapango ya Amboni,kimondo cha Mbozi na magofu ya Engaruka.
Akitoa sifa ya moja ya kivutio bwana Makombe amesema kuna kivutio cha mchanga unaohama kwa kati ya mita 15-17 kwa mwaka ukiwa na umbo la nusu mwezi bila kuachana ambapo watalii wengi hufika kuona maajabu hayo.
Ameeleza jamii katika eneo hilo huamini mchanga wa eneo hilo ni tiba kwa mahusiano yaliyolegalega na kuwataka wasweden kutembelea Tanzania ili kujionea maajabu hayo.
Hifadhi ya Ngorongoro pia imepambwa na utamaduni wa kihistoria ambapo eneo la jiopaki ya Ngorongoro Lengai kuna makabila ya wahadzabe na wadatoga ambapo makabila hayo bado yanaheshimu mila na utamaduni wao bila kuathiriwa na mila nyingine.

0 Comments