NA MWANDISHI WETU
Chama Cha ACT Wazalendo Jana Juni 14, 2025 kimezindua kampeni ya OKTOBA LINDA KURA inayolenga kuwahamasisha wananchi kupiga na kulinda kura zao.
Akifafanua malengo ya Kampeni hiyo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Mwembeyanga, Temeke, Dar es salaam, Katibu Mkuu wa Chama hicho Ado Shaibu alisema kuwa lengo la kampeni hiyo ni kuhamasisha umma kutekeleza wajibu wake wa kimapambano wa kupiga na kulinda kura kwa nguvu zote.
"Mmesikia mengi. CCM wamewaeleza Oktoba wanatiki. Kwamba licha ya umaskini, utekaji na huduma mbovu za kijamii wao hawajali, wanatiki. Chadema wamesema wana No Reforms No Election. Msimamo wetu rasmi ni kuwa tunaheshimu mawazo ya Chadema kwa sababu nayo ni njia ya mapambano. Sisi ACT Wazalendo tumekuja na kampeni ipi? ACT tunasema baada ya kupiga kura, umma una kazi ya kulinda kura ndio maana tumekuja na kampeni ya Oktoba Linda Kura," alisema Ado.
Naye Kiongozi wa Chama hicho Dorothy Semu alisema kuwa ACT Wazalendo imeamua kuingia kwenye Uchaguzi baada ya kujiridhisha kuwa kususia kutainufaisha sana CCM. Alisema kuwa uzoefu duniani kote unaonesha kuwa wanamageuzi waliokuwa na hali kama yetu hawakususia uchaguzi, waliendeleza mapambano.
Mwanachama mpya wa ACT Wazalendo ambaye pia ni Katibu wa Shura ya Maimamu Sheikh Ponda Issa Ponda alisema kuwa wananchi ni lazima wasimame imara kwa kupiga kura kwa wingi kwa ACT Wazalendo lakini pia kuzilinda kura hizo. Aliwahamasisha wananchi kuwa baada ya kupiga kura wasikae mbali na vituo vya kupigia kura.

0 Comments