Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Irene Gowelle akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 19, 2025 jijini Dar es Salaam.
NA ABRAHAM NTAMBARA, DAR ES SALAAM
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) limetangaza kuanza kwa kampeni maalum ya kuhamasisha ulipaji wa madeni kutoka kwa wateja wa malipo ya baada na ukaguzi wa mita za Luku kwa wateja wa malipo kabla.
Hayo yamebainishwa na leo Juni 19, 2025 na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma TANESCO Irene Gowelle, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Gowelle aamesema kuwa kampeni hiyo imeanza leo Juni 19 , 2025 ambapo imepewa jina la “Lipa Deni, Linda Miundombinu, Tukuhudumie” ikienda sambamba na kauli mbinu isemayo “Huduma endelevu huanza na wewe”.
Ameeleza kuwa zoezi hilo litaenda sambamba na kuhamasisha ulinzi wa miundombinu ya umeme ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha na kuimarisha uendelevu wa upatikanaji wa huduma bora ya umeme kwa wananchi.
“Malengo ya kampeni hii kuwahamasisha wateja wa malipo ya baada ya kulipa madeni yao kwa hiyari kabla ya hatua za kisheria kuchukuliwa na kutoa motisha kwa ulipaji wa wakati ikiwemo msamaha wa riba kwa wateja watakaolipa madeni yao kikamilifu,” amesema Gowelle.
Ameeleza kuwa katika kampeni hiyo itahusisha ukaguzi wa mita za luku kwa lengo la kuhakikisha zinafanya kazi vizuri na hazijachezewa na wateja wasio waaminifu.
Gowelle amesema kuwa watahamasisha umuhimu wa ulinzi shirikishi wa miundombinu ya umeme kwa kuwajumuisha wananchi na kuwapa elimu ya kulinda miundombinu ya shirika.
Ametoa rai kwa wateja wake nchini ambao wanadaiwa kutoa ushirikiano kwa kilipa madeni yao kwa wakati na hivyo kutoathiri upatikanaji wa huduma ya umeme kwenye shughuli zao.
“Tunatoa rai kwa wananchi kutoa taarifa kuhusu vitendo vya wizi wa umeme au uharibifu wa miundombinu kwa kushirikiana na vyombo vya dola ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza kwa ukosefu wa huduma ya umeme pamoja na kuzuia hasara kwa shirika,” ameeleza Gowelle.


0 Comments