Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Chama cha ACT Wazalendo kimedai kuwa Jeshi la Polisi na baadhi ya Wakuu wa Wilaya kuanza kuwasiliana na viongozi wa chama hicho kuwataka wawasilishe majina ya watia nia wa Ubunge na Udiwani.
Hayo yamebainishwa leo Julai 10 na Katibu Mkuu wa Chama hicho Ado Shaibu akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Saalam ambapo amelaani kitendo phicho.
Kwa mujibu wa Shaibu, maeneo yaliyoripotiwa kuhusika na mawasiliano hayo yasiyo ya kisheria ni pamoja na Kilwa, Kigamboni, Kinondoni, Magu na Tarime.
Hivyo ameeleza kuwa hakuna msingi wa kisheria unaolazimisha chama cha siasa kuwasilisha taarifa za wagombea kwa Jeshi la Polisi au Wakuu wa Wilaya.
"Hatua hiyo ni kinyume na sheria za uchaguzi na inalenga kuwatisha au kuwadhoofisha wagombea wake. “Hatua hii ya Jeshi la Polisi haina nia njema kwenye mchakato wa uchaguzi,” amesema Shaibu.
Kwamba kufuatia jambo hilo hatua walizochukua ni pamoja na kumuandikia barua Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali Camilius Wambura, kutaka kusitisha mara moja zoezi hilo ambalo wamelitaja kuwa ni haramu.
Kadhalika Chama hicho kimewasilisha malalamiko kwa Msajili wa Vyama vya Siasa na kutaka hatua zichukuliwe dhidi ya vitendo vya Jeshi la Polisi na Wakuu wa Wilaya.
Kwmaba wameagiza viongozi wa ACT Wazalendo nchini kote kutotoa taarifa zozote kuhusu wagombea kwa Jeshi la Polisi.
Pamoja na hayo ACT Wazalendo imeiandikia Tume ya Uchaguzi (INEC) kuitaka kutoa tamko rasmi dhidi ya uingiliaji huo wa Polisi kwenye mchakato wa uteuzi wa ndani wa vyama.
Hata hivyo kufuatia tuhuma hizo Jeshi la Polisi, kupitia taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo Julai 10, 2025 na Msemaji wake Makao Makuu imetoa ufafanuzi kuhusu madai hayo ya Katibu Mkuu wa Chama hicho kwamba wamemwandikia barua Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini kuhusu tuhuma hizo ambapo taarifa hiyo imeeleza kuwa barua hiyo haijamfikia IGP.
Aidha imeeleza kuwa endapo itamfikia maudhui yake yatafanyiwa kazi kwa haraka ili kupata ukweli wake na mawasiliano hayo yametoka wapi na yametolewa.

0 Comments