Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesisitiza umuhimu wa kudumisha misingi ya haki, amani, umoja na mshikamano kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Akizungumza katika Kongamano la Amani lililoandaliwa na Umoja wa Maimamu Tanzania (UMATA) na Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania, Rais Samia amesema uchaguzi ni fursa ya kidemokrasia inayopaswa kuendana na utulivu wa taifa.
“Kudumisha amani ni utamaduni wetu katika demokrasia ya uchaguzi. Tuulinde kabla, wakati na baada ya uchaguzi,” amesema Rais Samia.
Ametoa wito kwa viongozi wa dini, jamii na siasa kushirikiana kuhubiri amani, hasa wakati huu ambapo joto la kisiasa huongezeka. Amesisitiza kuwa ushirikiano wa makundi haya utasaidia kuzuia migongano isiyo ya lazima.
Rais Samia amewaonya wanasiasa dhidi ya lugha za uchochezi na kuwataka wajikite katika sera na hoja zenye kujenga taifa. Vilevile, amesisitiza utii kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na ushirikiano na vyombo vya ulinzi na usalama.
Kwa upande wa vyombo vya habari, Rais Samia amesema waandishi wana nafasi ya kipekee katika kulinda au kuhatarisha amani ya nchi kupitia taarifa wanazotoa. Ameeleza kuwa serikali inaendelea kukuza sekta ya habari ili kuongeza uwazi na uhuru wa kujieleza.
Akihitimisha, ametoa wito kwa Watanzania kujitokeza kwa wingi kupiga kura Oktoba 29, 2025, akisisitiza kuwa ni wajibu wa kizalendo na kikatiba kwa kila raia.
0 Comments