Mkinga, Tanga
Mgombea urais kupitia Chama cha NLD, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa chama hicho, Mhe. Doyo Hassan Doyo, ameendelea na ziara yake ya kampeni katika Wilaya ya Mkinga, mara baada ya uzinduzi rasmi wa kampeni za uchaguzi.
Akiwa katika mikutano iliyofanyika kijiji cha Mtimbani na Moa, Mhe. Doyo aliwahutubia wananchi na kusisitiza kuwa wakazi wa ukanda wa pwani ya Bahari ya Hindi wamesahauliwa na serikali iliyopo madarakani. Aliwaahidi kwamba endapo watampa ridhaa ya kuongoza nchi, atahakikisha ananunua meli kubwa zitakazosaidia wavuvi na vijana wa eneo hilo kupata ajira, sambamba na kufungua vituo vya usindikaji wa samaki ndani ya Wilaya ya Mkinga.
“Pamoja na hali ngumu mnayopitia, bado nyavu zenu mnachomewa badala ya kuwekewa mazingira mazuri ya uvuvi. Mkinipa ridhaa, nitahakikisha viwanda vya kusindika samaki vinajengwa katika ukanda huu ili vijana wapate ajira na kuuza bidhaa zao, ikiwemo samaki, kwa fedha za kigeni,” alisema Mhe. Doyo.
Kwa upande wake, Meneja wa Kampeni wa mgombea huyo, Ndugu Pogora Ibrahim Pogora, aliwataka wananchi wa Mkinga kutumia nafasi ya uchaguzi huu kuleta mabadiliko, akibainisha kuwa kosa si kufanya mabadiliko, bali ni kuridhika na maisha magumu yanayozidi kuleta majuto. “Tunawaomba wananchi msifanye makosa. Ili heshima yenu irudi, ni lazima kuleta mabadiliko kupitia kura zenu. Mpeni kura zote Mhe. Doyo ili aweze kushughulikia changamoto zenu,” alisema Pogora.
Kampeni za Chama cha NLD zinaendelea, ambapo baada ya mkutano wa leo Mkinga, msafara wa kampeni unatarajiwa kuelekea Wilaya ya Muheza na baadaye Korogwe.
0 Comments