Na Mwandishi Wetu, Longido
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Makalla, ametoa wito kwa viongozi na watendaji wa Wilaya ya Longido kuendelea kudumisha amani na utulivu wakati taifa likielekea katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani mwaka huu.
Akizungumza katika ukumbi wa J. K. Nyerere wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido na watumishi wa Halmashauri, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya pamoja na viongozi wa mila, CPA Makalla amewataka watendaji kuwafikia wananchi moja kwa moja ili kutatua changamoto na migogoro iliyopo kwa wakati.
Amesema kuwa jukumu la viongozi wa serikali na mila ni kushirikiana kuhakikisha wananchi wanapata elimu ya uchaguzi, ili waweze kutumia haki yao ya msingi ya kuchagua viongozi wanaowataka kwa uhuru na amani.
“Ni wajibu wetu kuhakikisha wananchi wanapiga kura kwa amani, bila hofu wala vikwazo. Tushirikiane kutatua migogoro, kudumisha mshikamano na kulinda utulivu kwa maslahi ya maendeleo ya taifa letu,” alisema CPA Makalla.
Kwa upande wake, Kiongozi wa Mila, Bw. Lekule Laizer, alisisitiza dhamira ya viongozi wa kimila kushirikiana na serikali katika kuimarisha mshikamano na kudumisha amani, hususan katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi.
“Viongozi wa mila tumejipanga kushirikiana bega kwa bega na serikali kuhakikisha wananchi wetu wanaishi kwa amani, migogoro inatatuliwa mapema na kila mmoja anatimiza wajibu wake kwa maslahi ya wilaya na taifa kwa ujumla,” alisema Bw. Laizer.
Aidha, CPA Makalla aliongeza kuwa ushirikiano wa karibu baina ya viongozi wa mila, Kamati ya Ulinzi na Usalama pamoja na watumishi wa serikali utasaidia kuimarisha mshikamano wa kijamii na kulinda amani ambayo ni msingi wa demokrasia na maendeleo.
0 Comments