UNFPA: WAANDISHI WA HABARI NI NGUZO MUHIMU KUFANIKISHA UTEKELEZAJI DIRA YA MAENDELEO YA TAIFA 2050


NA MWANDISHI WETU

SHIRIKA la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) limesema  wandoshi wa habari nchini  ni nguzo muhimu katika kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 (TDV 2050), kwa kusaidia kuielewa, kuifikisha kwa wananchi, na kuifanya kuwa nyenzo ya mabadiliko ya kijamii na kiuchumi.

Hayo yamebainishwa  leo Agosti 19, 2025 Naibu Mwakilishi na Afisa Mkuu wa UNFPA nchini, Melissa Barrett, wakati wa  mafunzo maalum kwa waandishi wa habari yaliyoandaliwa na UNFPA kwa kushirikiana na Tume ya Mipango jijini Dar es Salaam.

Amesema waandishi wa habari wana nafasi ya kipekee ya kuibua simulizi zenye kuhamasisha, kukuza uelewa wa wananchi kuhusu dira hiyo na kuhakikisha kunakuwepo na uwajibikaji wa wazi katika utekelezaji wake.

Melissa amesisitiza kuwa kwa kutumia majukwaa ya jadi na yale ya kidijitali, wanahabari wana uwezo wa kuifikisha TDV 2050 kwa lugha rahisi na yenye mvuto kwa jamii yote.

“Mafunzo haya si tu yanapanua uelewa wa wanahabari kuhusu maudhui ya dira hii, bali yanajenga ushirikiano thabiti kati ya serikali, vyombo vya habari, na washirika wa maendeleo na kazi ya waandishi si kuripoti tu, bali pia kuwaelimisha wananchi, hasa vijana, kuhusu fursa lukuki zitakazotokana na utekelezaji wa dira hii,”amesema.


Kwa upande wake, Naibu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Mursali Milanzi, amesema kuwa maandalizi ya utekelezaji wa TDV 2050 yameanza kwa kuwajengea uwezo waandishi wa habari, ili wawe mabalozi wa kuelezea dira hiyo kwa wananchi kwa usahihi.

Ameongeza kuwa utekelezaji wa dira hiyo unatarajiwa kuanza rasmi mwaka wa fedha wa 2026/2027.

Milanzi amefafanua kuwa dira hiyo imejikita kwenye nguzo kuu tatu: ukuaji wa uchumi, maendeleo ya watu, na utunzaji wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Alieleza kuwa serikali tayari imeweka mifumo madhubuti ya ufuatiliaji na uwajibikaji, itakayosimamiwa na Tume ya Mipango ili kuhakikisha dira hiyo inaleta matokeo chanya.

Pia ameahidi kuwa serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na vyombo vya habari katika kutoa elimu na taarifa sahihi kuhusu dira hiyo, ili kila Mtanzania, kuanzia ngazi ya kaya hadi taifa zima, aweze kushiriki kikamilifu katika safari ya kuelekea maendeleo endelevu ya mwaka 2050.

Post a Comment

0 Comments