VIJANA WAZALENDO WAAHIDI KUKABILINA NA WANAOPANGA KUTUMIA UCHAGUZI MKUU KUVURUGA AMANI, wasema watamlinda na kumtetea Rais Samia



NA MWANDISHI WETU

MWENYEKITI wa Kampeni ya Mama Asemewe na Rais wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO), Geofrey Kiliba amesema Vijana wazalendo wa Tanzania watakabiliana na yeyote anayepanga kutumia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 kwa ajili ya kuvuruga amani ya Nchi.

Kiliba ametoa kauli hiyo leo Agosti 18, 2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam ambapo amesisitiza umuhimu wa kukabiliana kisera badala ya kushambuliana na kuhatarisha tunu za Taifa la Tanzania.
 
Ametumia fursa hiyo kuahidi kuwa vijana wamekula kiapo cha kupambana na wale wote wasioitakia mema Tanzania na wanaotaka kusambaratisha amani, utulivu na mshikamano wa Tanzania.

"Kwa imani hii, tutamtetea, tutamlinda Kiongozi ama Mtanzania anayefanya vizuri kwaajili ya Taifa hili. Kwa imani hii tutashambulia kila Mtanzania mwenzetu anayedhani hawezi kukabiliana na sera, ilani, maono na malengo ya mgombea akaamua kukabiliana na mtu binafsi. Tutashambulia na kushambulia kwetu tutawaeleza watanzania juu ya nia yako ovu, watanzania wajue," amesema Kiliba.

Amewataka Wazee waliopambana kulipigania Taifa la Tanzania kuwa na imani na Vijana wa sasa, akieleza kuwa wapo tayari kuhakikisha Tanzania inabaki salama kwaajili ya kizazi cha leo na cha kesho hasa kwa kuzingatia misingi na tunu zilizoachwa na waasisi wa Tanzania na wazee waliopambana kuhakikisha Tanzania inakuwa na umoja, amani, utulivu na mshikamano.

Katika hatua nyingine Kiliba amehoji uhalali wa baadhi ya wananchi wanaomtusi na kutoa lugha za fedheha kwa Viongozi wa Serikali akiwemo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, akisisitiza umuhimu wa kuwaheshimu na kuwalinda Viongozi wa serikali.

Akibainisha mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha miaka minne ya Rais Samia wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar Es Salaam leo Jumatatu Agosti 18, 2025, Kiliba ameeleza kuwa ni muhimu kwa wanaowatusi Viongozi kuacha mara moja na kueleza kuhusu Kiongozi wanayemtaka kuweza kuwaongoza tofauti na Rais Samia.

"Imefikia hatua wale tuliokuwa tunawaamini, kuwatumaini na kuwategemea, wameanza kuwekeza fedha kwaajili ya matusi, tumefikia hatua hiyo, kosa ni lipi? Kwa mazuri na kazi nzuri aliyoifanya Dkt. Samia kwa kipindi hiki tutamlinda na kumtetea. Sisi watanzania tunahitaji maendeleo na huduma bora za kijamii na kadhalika sasa tunamkataa ili tumlete mtu wa namna gani wa kufanya vitu tofauti na hivyo?," amehoji Kiliba.

Kiliba amempongeza Rais Samia pia kwa kufanikisha miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo mradi wa reli ya kisasa SGR, Bwawa la kuzalisha umeme la Mwalimu Nyerere, Ujenzi wa mtandao mkubwa wa barabara kwa Kiwango cha lami, umeme wa uhakika na udhibiti wa mfumuko wa bei nchini, akisema masuala hayo yamekuwa chachu ya maendeleo kwa Watanzania.

Amebainisha, vijana watakabiliana vilivyo na aliyekuwa Mbunge wa Kawe Askofu Josephat Gwajima ikiwa ataendelea kwenda kinyume na taratibu na Miongozo yenye kuwaongoza Viongozi wa dini nchini.

Kiliba amekiri kuwa aliwahi kuwa muumini wa Askofu Gwajima na sasa anashangazwa na kauli za vitisho zinazotolewa na Kiongozi huyo wa kidini kwa Viongozi wa serikali.

"Kiongozi wa dini anakuambia baada ya siku kadhaa atazungumza jambo ambalo litamstaajabisha kila mtu? Mnatufundisha nini? kama Kiongozi wa dini uko hivyo sisi Vijana tutajifunzia wapi upole na ukarimu? Hapana, tunachukua hatua kubwa sana ya maneno yetu lakini tusilazimishane kutojali ama kutochukua hatua za tahadhari tunapowazungumzia Viongozi wa dini," amekaririwa Bw. Kiliba.

Kiliba ameahidi kuwa ikiwa Askofu Gwajima atajitokeza mbele ya wanahabari ndani ya siku kumi zijazo kama alivyoahidi naye atarejea tena kwa waandishi wa habari, akieleza kuwa sasa atamkabili Kiongozi huyo wa kidini bila kujali nafasi aliyonayo katika uongozi wa kidini, akibainisha kuwa haiwezekani mtu mmoja akatishia amani na mshikamano uliopo nchini.

Post a Comment

0 Comments