𝗖𝗖𝗠 𝗞𝗨𝗭𝗜𝗡𝗗𝗨𝗔 𝗛𝗔𝗥𝗔𝗠𝗕𝗘𝗘 𝗬𝗔 𝗞𝗜𝗧𝗔𝗜𝗙𝗔 𝗞𝗨𝗖𝗛𝗔𝗡𝗚𝗜𝗔 𝗞𝗔𝗠𝗣𝗘𝗡𝗜, yalenga kukusanya shilingi milioni 100




NA MWANDISHI WETU

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, amesema 𝗖𝗖𝗠 imeweka lengo la kukusanya Shilingi Bilioni 100 kupitia harambee ya kitaifa itakayozinduliwa rasmi kesho saa 11 jioni katika Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.

Akizungumza na wahariri na waandishi wa habari katika ofisi ndogo za CCM Makao Makuu, Lumumba mkoani Dar es Salaam, leo tarehe 11 Agosti, 2025, Dkt. Nchimbi amesema uamuzi wa kuandaa harambee hiyo umetokana na hamasa kubwa iliyojitokeza kwa wanachama wa CCM kutaka kuchangia kampeni.

“Kwa wakati ule kulitokea hamasa kubwa kwa wanachama wa CCM kutamani kuchangia michango ya kampeni. Kutokana na hamasa hiyo, sisi kama Kamati Kuu tumeamua sasa kuwashirikisha wanachama wetu katika uchangiaji kesho saa 11 jioni katika ukumbi wa Mlimani City,”

Aidha, Dkt. Nchimbi ameeleza malengo ya kuchangia, ambapo amesisitiza kuwa;

“Tunachokusudia kupata kwa kiwango cha kawaida ni Bilioni 100. Wanasiasa kokote walipo wajue hiyo ndiyo target tunayokusudia.”

Vilevile, Dkt. Nchimbi amefungua milango kwa vyama vingine kuchangia katika kampeni hiyo ambapo amesema kuwa;

“Kuhusu vyama vingine, tutafarijika sana vikichangia, kwa sababu haihitaji ushahidi wa kipolisi kujua CCM inatumikia Watanzania na vyama vingine vyote.”

Akizungumzia kuhusu udhibiti wa fedha haramu, Dkt. Nchimbi amesema “Jitihada yetu kubwa sisi kama CCM ni kujiepusha kuwa Serikali, kwa hiyo sisi siyo taasisi ya uchunguzi wa fedha haramu. Wenye kazi yao wataendelea kutafuta fedha hizo, sisi tutaendelea kufanya kazi ya siasa, kwa maana kitu kinachoharibu nchi ni chama cha siasa kuendelea kufanya kazi za dola.”

Harambee hiyo inatarajiwa kuongozwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya chama hicho kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Post a Comment

0 Comments