BRELA YATOA TUZO KWA MHITIMU BORA WA JUMLA WA CHUO KIKUU MZUMBE KAMPASI YA MOROGORO


Bi Theresa Chilambo, Afisa Habari na Mawasiliano Mkuu kutoka Wakala wa Usajili na Leseni (BRELA) akikabidhi mfano wa Hundi kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA Bw Godfrey Nyaisa kwa Bi Melina Baradyana mhitimu bora wa jumla aliyepata wakia ya 4.8 kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe kampasi ya Morogoro. Bi Melina Baradyana ni mhitimu wa Shahada ya Usimamizi wa Mazingira.

Mhe Philemon Luhanjo, Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu akitoa tuzo ya cheti kwa Bi Melina Baradyana mhitimu bora wa jumla kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe kampasi ya Morogoro aliyepata wakia ya 4.8. Bi Melina Baradyana ni mhitimu wa Shahada ya kwanza katika Usimamizi wa Mazingira.

NA MWANDISHI WETU  

Wakala wa Usajili wa Leseni na Biashara (BRELA) imetoa tuzo kwa mhitimu bora wa jumla wa mwaka 2025 kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe kampasi ya Morogoro

Tuzo hiyo imetolewa tarehe 19 Novemba, 2025 kwa Bi. Melina Baradyana aliyetimu shahada ya kwanza katika Usimamizi wa Mazingira na kuibuka mwanafunzi bora wa jumla kwa wahitimu wote wa shahada ya kwanza kutoka kampasi ya Morogoro kwa mwaka 2025 kwa kupata wakia (GPA) ya 4.8 

Akifungua hafla hiyo Mhe Philemon Luhanjo, Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu amesisitiza kuwa wahitimu wa Mzumbe wawe chachu ya kurudisha maendeleo kwa chuo hicho kwa kutunisha mfuko maalum wa wahitimu kutoka Mzumbe ili kwa elimu waliyonufaika nayo iweze kuleta mchango kwa wanafunzi wenye changamoto na maboresho ya mazingira ya chuo hicho

Nae, Bi Melina Baradyana mnufaika wa Tuzo hiyo ameishukuru BRELA kwa kutambua juhudi zao kwani itatoa hamasa ya ushindani kwa wanafunzi wengine waendelee kufanya bidii katika masomo

"Asante sana BRELA kwa mchango huu, itanisaidie kuendelea na masomo yangu ya Shahada ya Uzamili hapahapa Mzumbe na fedha hizi zitanisaidia kufanikisha kwenye tafiti zangu ninazozifanyia kazi" ameeleza Bi Baradyana

BRELA imetoa tuzo ikiwa ni muendelezo wa mashirikiano na Chuo Kikuu Mzumbe ambapo kwa  Mwaka 2025 ufadhili wa Tuzo kwa Mhitimu wa Jumla imetolewa kwa Kampasi ya Morogoro,  tarehe 27 Novemba, 2025 itatolewa kwa mhitimu kampasi ya Mbeya  na tarehe 4 Desemba, 2025 itatolewa kwa mhitimu bora kampasi ya Dar es Salaam 

Hafla ya utoaji wa tuzo hizo zimehudhuriwa pia na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe Profesa William Mwegoha, wahadhiri, wahitimu na wanafunzi wa chuo hicho

Post a Comment

0 Comments