NA ABRAHAM NTAMBARA, LONGIDO
Serikali
imetenga shilingi milioni 600 kwa ajili ya kuboresha Bwawa la Kijiji cha
Kiserian, ikiwa ni hatua ya kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji katika
eneo hilo.
Hayo
yamebainishwa hivi karibuni na Mkuu wa Wilaya ya Longido, Mhe. Salum Kalli,
wakati alipokuwa akizungumza na wananchi alipotembelea mnada wa Soko la
Kiserian, Kata ya Engikaret.
“Serikali
imeleta shilingi milioni 600. Tunakwenda kuboresha bwawa hili, tunataka
kulifukua ili mpate maji ya uhakika. Bwawa hili litamaliza kero ya maji,”
alisema Mhe. Kalli.
Aliongeza
kuwa maboresho hayo yataanza hivi karibuni, huku akiwahakikishia wananchi kuwa
utekelezaji wa mradi huo utafanyika kwa haraka ili kuhakikisha maji yanapatikana
mapema.
Katika
hatua nyingine, Mhe. Kalli alisema kuwa Serikali ina mpango wa kuboresha mnada
wa Soko la Kijiji cha Kiserian kwa lengo la kuufanya ufanyike kila siku, badala
ya kufanyika siku moja tu ya Ijumaa.
Alisema
kuwa maboresho hayo, yakikamilika, yatawezesha wananchi kufanya biashara muda
wote, kuongeza kipato chao na hivyo kuboresha maisha ya familia zao.
Mhe. Kalli alitumia pia fursa hiyo kuwapongeza wananchi kwa kushiriki uchaguzi kwa amani na kumchagua Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ushindi mkubwa wa kishindo.
0 Comments