NA ABRAHAM NTAMBARA, LONGIDO
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Bw. Nassor Shemzigwa, leo Disemba 3, 2025 amekabidhi vyeti vya ardhi kwa vijiji vitano vya Halmashauri hiyo.
Mradi huu umewezeshwa na Shirika lisilo la Kiserikali la Ujamaa Community Resource Team (UCRT) kwa ushirikiano na Halmashauri ya Wilaya ya Longido chini ya ufadhili wa IWIGIA.
Akizungumza baada ya makabidhiano hayo, Msimamizi wa UCRT kwa upande wa Longido Bw. Paulo Rokonga amevitaja vijiji hivyo kuwa ni Matale B, Orgirha, Oltepes, Wosiwosi na Orpukel.
“Makabidhiano haya yanafanyika baada ya kukamilika kwa zoezi la upimaji wa vijiji, uandaaji wa vyeti vya ardhi na usuluhishi wa migogoro ya mipaka ya vijiji,” amesema Bw. Rokonga na kuongeza:
“Mfano, kulikuwa na mgogoro kati ya vijiji vya Matale B na Wosiwosi. Vijiji hivi vilikubali kupimiwa upya maeneo yao, na sasa wamekabidhiwa nyaraka zao zilizopimwa upya.”
Bw. Rokonga ametaja nyaraka zilizokabidhiwa kuwa ni pamoja na vyeti vya ardhi, hati za kimila za nyanda za malisho, daftari la kumbukumbu la usajili wa vyeti vya ardhi pamoja na mihuri ya moto.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Orgirha, Kata ya Mundarara, Tarafa ya Engarenaibor, Bw. Lekeni Laizer, akizungumza kwa niaba ya viongozi wa vijiji hivyo, ameishukuru Serikali pamoja na Shirika la UCRT kwa kuwakabidhi nyaraka hizo.
Bw. Laizer amesema kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kumaliza na kukomesha migogoro ya ardhi
katika vijiji vyao.
0 Comments