*ASISITIZA USHIRIKIANO WA KIKANDA KUKABILIANA NA HALI HIYO
*ATOA WITO WA ELIMU KUENDELEA KUTOLEWA KWA WANANCHI JUU YA MATUMIZI SAHIHI YA DAWA
NA MWANDISHI WETU
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amesema Tanzania imedhamiria kuhakikisha inalinda afya, maisha ya watu na mazingira kwa kutoa kipaumbele katika uimarishaji wa mfumo wa afya, kuwekeza katika utafiti wa kisayansi, na kuhimiza matumizi ya dawa kama yanavyokusudiwa kwa manufaa ya watanzania na dunia kwa ujumla.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akifungua Maadhimisho ya Kanda ya Afrika ya Wiki ya Kimataifa ya Usugu wa Vimelea vya Magonjwa dhidi ya Dawa, yanayofanyika Hyatt Regency, Jijini Dar es Salaam. Amesema hatua hizo ni katika kukabiliana na tishio linaloongezeka la usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa, ambapo pia ametoa wito kwa nchi za Afrika kujiunga katika mapambano hayo ya kimataifa kwa kuunga mkono juhudi za matumizi sahihi ya dawa hizo za kuokoa maisha, kwa kubadilishana ujuzi, kuimarisha ushirikiano na kuhakikisha kwamba dawa za vimelea vya magonjwa zinabaki kuwa na nguvu kwa vizazi vijavyo.
Halikadhalika, Makamu wa Rais amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa kupitia kubadilishana takwimu na uratibu wa utekelezaji wa sera katika mapambano dhidi usugu wa vimelea vya magonjwa. Amesema ushirikiano huo ni muhimu kwa kuwa maambukizo hayazuiliwi na mipaka ya kijiografia.
Vilevile, Makamu wa Rais amesema uwekezaji katika uvumbuzi na utafiti ni muhimu kwa lengo la kuboresha zana mpya za uchunguzi, chanjo na matibabu mbadala ambayo yanaweza kupunguza utegemezi kwa dawa za asili za vimelea vya magonjwa na kuweza kudhibiti mabadiliko ya magonjwa yanayojitokeza kwa jamii moja moja.
Pia, Makamu wa Rais ametaja umuhimu wa utoaji elimu kwa umma na ushirikishwaji wa jamii ili kuwezesha wananchi kufuata ushauri wa huduma ya afya, kukamilisha dawa zilizoagizwa, kuepuka matumizi mabaya ya dawa za vimelea vya magonjwa na dawa zinginezo na kuzingatia viwango vya kuzuia na kudhibiti maambukizi.
Makamu wa Rais amesema licha ya mafanikio yaliyopatikana hadi sasa, Tanzania ina dhamira ya kuongeza juhudi za kukabiliana na usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa kupitia mipango mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji ili kuwa sera na afua zinazozingatia ushahidi.
Vilevile, kuongeza hatua za kuzuia na kudhibiti maambukizi kote katika huduma za afya, shamba na mazingira ya jamii ili kupunguza kuenea kwa magonjwa sugu, kuimarisha matumizi sahihi ya dawa za vimelea vya magonjwa katika sekta ya afya ya binadamu na wanyama, kutekeleza mifumo thabiti ya udhibiti na uangalizi ili kuzuia matumizi mabaya ya dawa za kuua vimelea vya magonjwa, pamoja na kuendeleza utafiti, uvumbuzi, na suluhu mbadala ili kuwa na ufanisi wa dawa.
Maadhimisho hayo yanayofanyika tarehe 2 hadi 5 Desemba 2025 yanashirikisha wadau mbalimbali wa sekta ya afya Barani Afrika yakiwa na kauli mbiu isemayo “Chukua hatua sasa: Ilinde leo, kuwa na kesho salama”
0 Comments