LONGIDO YAWEKA MIKAKATI YA KUIMARISHA UFAULU NA KUBORESHA ELIMU MWAKA 2026







NA MWANDISHI WETU, LONGIDO

Halamshauri ya Wilaya ya Longido Januari 23, 2026 imefanya kikao kazi na Wakuu wa Shule za Sekondari wilayani humo kwa lengo la kujadili na kuweka mikakati ya kuimarisha ufaulu na kuboresha utoaji wa elimu kwa mwaka wa masomo 2026.

Kikao hicho kilichofanyika katika Shule ya Sekondari Longido kililenga kufanya tathmini ya hali ya elimu na kuweka mikakati madhubuti ya kuinua viwango vya ufaulu, hususan kwa wanafunzi wa Kidato cha Pili na cha Nne.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, Afisa Elimu wa Wilaya ya Longido, Mwalimu Gilbert Sombe, amesema kuwa kikao hicho kimejadili kwa kina mbinu mbalimbali za kuimarisha mchakato wa ufundishaji na ujifundishaji katika shule zote za sekondari wilayani humo.

Ameeleza kuwa mkutano huo umeweka msisitizo katika kuhakikisha wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Kwanza wanaripoti shuleni kwa wakati, sambamba na kuendelea kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuishi kwa wanafunzi ikiwemo upatikanaji wa madawati na vitanda vya kulalia.

Aidha, Mwalimu Sombe amewahimiza Wakuu wa Shule kuendelea kuwatambua wanafunzi wenye mahitaji maalumu ili waweze kupatiwa msaada unaohitajika utakaowawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za masomo.

“Nawapongeza Wakuu wa Shule na wadau wote wa elimu kwa juhudi na ushirikiano wanaouonyesha katika kuimarisha sekta ya elimu wilayani Longido. Ni muhimu kuendelea kushirikiana ili kuboresha ustawi wa wanafunzi wetu,” amesema Mwalimu Sombe.

Vilevile, amepongeza ushirikiano mzuri uliopo kati ya Wakuu wa Shule, wadau wa elimu na viongozi wa maeneo mbalimbali wakiwemo viongozi wa vijiji, ambao umechangia kuboreshwa kwa miundombinu ya shule ikiwemo upatikanaji wa madawati na vitanda.

Akitoa taarifa ya hali ya wanafunzi wa Kidato cha Kwanza walioripoti shuleni, Mwalimu Sombe amesema jumla ya wanafunzi 2,724 wamechaguliwa kujiunga na Kidato cha Kwanza mwaka 2026, kati yao wavulana ni 1,455 na wasichana 1,269.

Kwa ujumla, kikao hicho kinaonesha dhamira ya Halmashauri ya Wilaya ya Longido kuendelea kuimarisha sekta ya elimu.

Post a Comment

0 Comments