NA MWANDISHI WETU
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Longido imetoa elimu ya maadili, uadilifu na uwazi kwa Walimu Wakuu wa Shule za Sekondari wilayani humo, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuimarisha uongozi bora na uwajibikaji katika sekta ya elimu.
Elimu hiyo imetolewa leo Januari 23, 2026 na Afisa wa TAKUKURU Wilaya ya Longido, Bw. Erick Mkawe, alipokuwa akizungumza katika kikao cha Walimu Wakuu wa Shule za Sekondari kilichofanyika katika Shule ya Sekondari Longido, kilichoandaliwa na Halmashauri ya Wilaya ya Longido.
Akizungumza katika kikao hicho, Bw. Mkawe amesisitiza umuhimu wa walimu wakuu kuzingatia maadili ya utumishi wa umma na taaluma yao kwa kutekeleza majukumu kwa uaminifu na uwajibikaji.
“Ni muhimu kuzingatia maadili ya utumishi wa umma katika utekelezaji wa majukumu yenu. Muwe waaminifu na wawazi, hususan katika masuala ya usimamizi wa shule na miradi ya maendeleo,” amesema Bw. Mkawe.
Amefafanua kuwa uwazi kwa Mkuu wa Shule ni msingi muhimu wa uongozi bora, akisisitiza umuhimu wa kuwashirikisha walimu na wadau wengine wa elimu katika masuala mbalimbali yanayoendelea shuleni, ikiwemo utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Bw. Mkawe ameeleza kuwa fedha zinazotolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo zinapaswa kutumika kwa mujibu wa malengo yaliyokusudiwa, na kufuata taratibu zilizowekwa endapo kutahitajika mabadiliko katika matumizi.
Amesema utoaji wa elimu hiyo unalenga kuwajengea uwezo walimu wakuu ili kuimarisha uwajibikaji na kuwaepusha na changamoto za kisheria zinazoweza kujitokeza kutokana na matumizi yasiyo sahihi ya rasilimali za umma.
Kadhalika, ametoa wito kwa walimu wakuu kuendelea kuwashirikisha wananchi na wadau wa maeneo husika katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hatua itakayochangia kuongeza uwazi, uwajibikaji na umiliki wa miradi hiyo.


0 Comments