Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), katika kutekeleza majukumu yake ya kuweka mazingira bora na wezeshi kwa wafanyabiasha, leo tarehe 20 Februari, 2026 imeendelea kutoa mafunzo ya urasimishaji biashara kwa vijana, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuwawezesha kupata maarifa na ujuzi wa kukuza uchumi wao na taifa kupitia mifumo halali ya kisheria.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Afisa Usajili kutoka Kurugenzi ya Kampuni na Majina ya Biashara, Bi. Maryglory Mmari alisema BRELA inaendelea kusogeza huduma zake karibu na wananchi kupitia mafunzo mbalimbali, maonesho ya biashara, kliniki za biashara pamoja na utoaji wa huduma za papo kwa papo kwa kushirikiana na maafisa biashara wa halmashauri mbalimbali nchini.
Katika mafunzo hayo yaliyofanyika kwenye Ofisi za BRELA jijini Dar es Salaam na kuwahusisha vijana kutoka Asasi ya Convention Social Economic Empowerment (CSEE), wakiwemo wanafunzi wa vyuo vya Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo cha Diplomasia, Chuo Kikuu Cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS), Chuo cha Uhasibu Tanzania (TIA) pamoja na wajasiriamali wanaoshiriki programu ya Mzalendo Tour, Bi. Mmari alisisitiza juu ya umuhimu wa wafanyabiashara kurasimisha biashara zao.
“Huduma zote za usajili kwa sasa zinapatikana kwa njia ya mtandao kupitia mfumo wa ORS, ni muhimu kwa wajasiriamali kuwa na akaunti na nyaraka muhimu kabla ya kuanza mchakato wa usajili na baada ya usajili, mmiliki wa biashara atatakiwa kuzingatia wajibu wa kisheria ikiwemo kuwasilisha taarifa za kila mwaka, kufanya marekebisho ya taarifa inapobidi na kutoa taarifa za mabadiliko ya kampuni ndani ya muda uliopangwa kisheria.” alisisitiza Bi. Mmari.
Kwa upande wake, Afisa Leseni kutoka Kurugenzi ya Leseni, Bw. Lucas Mafuru, alieleza utofauti wa leseni za biashara kundi “A” na “B” huku akieleza kuwa Leseni za Biashara Kundi “A” zinatolewa na BRELA kutokana na sura yake kuwa ya Kitaifa na Kimataifa wakati leseni za kundi “B” zinatolewa na mamlaka za halmashauri kwa biashara zenye upeo wa ndani.
Naye Msaidizi wa Msajili Mwandamizi kutoka Kurugenzi ya Miliki Ubunifu BRELA, Bw. Nassoro Mtavu alizungumzia zaidi kuhusu umuhimu wa Miliki Ubunifu katika kukuza ubunifu wa vijana, akiwaeleza kuwa mvumbuzi hupewa Hataza endapo uvumbuzi wake unathibitisha kuwa na uwezo wa kutatua changamoto za kijamii au kiuchumi kwa njia ya ubunifu.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Asasi ya Convention Social Economic Empower (CSEE), Bi. Theresia Assey, alisema ziara yao katika ofisi za BRELA imelenga kuwawezesha vijana kupata maarifa yatakayowasaidia kuanzisha na kuendesha biashara zao kwa kuzingatia taratibu za kisheria, akibainisha kuwa vijana wamepata uelewa mpana kuhusu fursa zinazotokana na urasimishaji wa biashara ikiwemo kupata mikopo, kuaminika kisheria na kupunguza migogoro ya kibiashara inayotokana na kutokujua sheria.
Naye mwanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) na mwanachama wa Mzalendo Tour, Luis Erick, alisema mafunzo hayo yamewapa ujasiri wa kuendesha biashara kwa misingi sahihi, huku akitoa wito kwa vijana wenzao kuhakikisha wanasajili majina ya biashara zao BRELA kupitia mfumo wa usajili ili kuzilinda kisheria dhidi ya migogoro ya umiliki.
Mafunzo hayo ni muendelezo wa Mkakati wa Wakala kuwafikia vijana wengi zaidi kwa kuwapatia elimu kuhusu urasimishaji biashara zikiwemo taratibu za usajili wa majina ya biashara na kampuni, utoaji wa leseni za biashara kundi “A”, leseni za viwanda pamoja na huduma za miliki bunifu ikiwemo hataza.


0 Comments