Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
VIJANA wanaotaka kuwania nafasi mbalimbali za uongozi wameshauriwa wasome na kuijua vizuri historia ya nchi na ya waasisi wa Taifa lao na sio kukimbilia uongozi na kutaka kuitwa ‘Waheshimiwa’ ili hali kuna vitu hawavijui.
Akizungumza katika mahojiano maalum, Ofisi Kuu, CCM, Kisiwandui Mjini Unguja, Katibu wa Kamati Maalum NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi Uenezi na Mafunzo Komredi Khamis Mbeto Khamis alisema ni vema vijana wakaujua uongozi kabla hawajautaka.
Alisema kila kijana anataka aitwe mheshimiwa nae binafsi anapenda vijana washike uongozi kwani baada ya kuondoka wazee katika uongozi nani watashika nafasi zao lakini wanatosha?.
“Wazee kina karume wameondoka, je hatuwezi kuwa na Karume mwingine?” alihoji Mbeto na kuongeza kuwa ni lazima wasome kwa utashi wao waujue uongozi” alisema Mwenezi huyo.
Alibainisha kuwa ni lazima wajue nidhamu ya uongozi, wasome historia ya nchi yao na ya waasisi wa Taifa lao na katika kusoma watapata maarifa ya kujua ulimwengu unaendaje.
“Niwaombe vijana wasome sana, wasome historia yao, wasome ulimwengu unaendaje, wasome uongozi, nidhamu ya uongozi ikoje na kikubwa wasiwe waoga” alisema.
Alisema vijana wanatakiwa wanyooke kwenye misimamo yao na nyeupe waseme nyeupe, nyeusi waseme nyeusi na jambo hilo kuna ambao litawachukiza lakini historia itaandikwa.
Komredi Mbeto ambaye anaamini pia kuwa uongozi ni kipawa kutoka kwa Mungu anatanabaisha kuwa maarifa hupatikana kwa kusoma vitabu vya wanafalsafa mbalimbali ili kujua dunia inaendaje.
“Leo unamwalika kiongozi unamuambia ataje historia ya nchi yake au viongozi wa Taifa anaanza kutafuta maneno, anahangaika” alisema Mbeto.
Anabainisha kuwa kijana kutambua historia ya Taifa lake lilipotoka, lilipo na linapoenda ndio jambo linalojenga uzalendo.
Mwenezi huyo ambaye amepata kufanyakazi na marais takribani wote isipokuwa Baba wa Taifa, Hayati Julius Kambarage Nyerere wakiwa wajumbe wa NEC, anasema viongozi hao wote kaulimbiu yao ilikuwa nchi, uzalendo kwanza.
Mbeto anawahimiza vijana wachape kazi inapotokea wakapewa dhamana na waache kujipendekeza kwa viongozi na kuwafitinisha na kuwaumiza wenzao.

0 Comments