NA MWANDISHI WETU, LONGIDO
Watunza kumbukumbu, maafisa utumishi pamoja na wataalamu wa TEHAMA katika Halmashauri ya Wilaya ya Longido wamepatiwa mafunzo kuhusu Mfumo wa Ofisi Mtandao (e-Office) unaosimamia mawasiliano ya majalada na barua katika taasisi za umma.
Mafunzo hayo yamefanyika leo, Aprili 21, 2026, katika ukumbi mdogo wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, mkoani Arusha.
Mwezeshaji wa mafunzo hayo, Afisa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Bw. Joseph Masalu, amesema dhamira kuu ya Serikali ni kuhakikisha ofisi zote za Serikali na taasisi zake zinatumia mfumo huo.
Ameeleza kuwa mfumo wa e-Office ulianza kutumika rasmi mwaka 2018 katika taasisi za Serikali ili kukuza matumizi ya TEHAMA na kuboresha utendaji kazi.
“Niko hapa kwa lengo la kuwezesha matumizi ya mfumo wa e-Office. Ni dhamira ya Serikali kuona ofisi zote za Serikali na taasisi zake zinatumia mfumo huu. Ni mfumo rafiki unaotumiwa na watunza kumbukumbu katika kuhifadhi na kusimamia nyaraka,” amesema Bw. Masalu.
Amebainisha kuwa matumizi ya mfumo huo yanalenga kupunguza gharama za uendeshaji, kuongeza uwajibikaji na ufanisi ndani ya taasisi za Serikali, pamoja na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Aidha, mfumo huo unarahisisha mawasiliano ya majalada na barua, kusaidia kufanya maamuzi kwa wakati, na kuwezesha upatikanaji wa taarifa kwa haraka pindi zinapohitajika.
Bw. Masalu ameongeza kuwa mfumo huo tayari umeleta mafanikio makubwa, ikiwemo kupunguza upotevu wa nyaraka, kuimarisha uwajibikaji, na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku.
Kwa upande wake, mnufaika wa mafunzo hayo, Mtunza Kumbukumbu wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Bi. Hilda Mbwambo, amesema mfumo huo utarahisisha upatikanaji wa majalada kwani kwa kutumia kompyuta mtumiaji ataweza kubaini kwa urahisi yalipo.
Ameongeza kuwa mfumo huo pia utaimarisha usiri wa nyaraka, tofauti na mfumo wa awali ambapo ilibidi mtu kupitia nyaraka nyingi ili kupata taarifa inayohitajika.







0 Comments