NA MWANDISHI WETU, LONGIDO
Mkuu wa Wilaya ya Longido, Mhe. Salum Kalli, leo Mei 26, 2026 ametembelea na kujionea maendeleo ya ujenzi wa madarasa mawili katika Shule Shikizi ya Ongong’u Osinyai iliyopo Kijiji cha Engikaret, Kata ya Engikaret wilayani Longido mkoani Arusha.
Akizungumza baada ya kukagua mradi huo ambao umefikia hatua ya kupaua, Mhe. Kalli amewapongeza viongozi wa kijiji na kata wakiongozwa na Diwani wa Kata ya Engikaret, Mhe. Mathayo Ndaiya Laizer, kwa usimamizi mzuri wa utekelezaji wa mradi huo.
“Madarasa haya ni makubwa na mazuri. Mwenyekiti mmefanya kazi nzuri sana kwani kama viongozi mlikaa mkakubaliana na kuutekeleza mradi huu vizuri,” amesema Mhe. Kalli.
Amesema shule hiyo itasaidia kutoa huduma ya elimu kwa watoto wa eneo la Engikaret na kuwapunguzia adha ya kutembea umbali mrefu kufuata masomo.
Aidha, amewahakikishia viongozi wa Kata na Kijiji cha Engikaret kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nao kuhakikisha ujenzi wa shule hiyo unakamilika kwa wakati ili wanafunzi waanze kunufaika na huduma hiyo muhimu.
Pamoja na hayo, Mhe. Kalli ameshauri viongozi hao kuwashirikisha wadau wa maendeleo waliopo katika eneo hilo ili kusaidia kukamilisha ujenzi huo kwa haraka zaidi.
Shule Shikizi ya Ongong’u Osinyai inajengwa kwa nguvu za wananchi kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Longido, Dkt. Steven Kiruswa.
0 Comments