SERIKALI YAENDELEA KUTENGA MAENEO MAPYA KWA WACHIMBAJI WADOGO, LESENI 108 ZATOLEWA


✔️Deni la Bilioni 1.52 la Waliokuwa Wafanyakazi wa Kiwira Kulipwa Baada ya Uhakiki wa Mwisho

📍Dodoma,– 

Serikali imeendelea kuimarisha mazingira ya uwekezaji na ushiriki wa wananchi katika Madini kwa kuendelea kutenga maeneo maalum kwa ajili ya wachimbaji wadogo nchini, hatua inayolenga kuongeza fursa za ajira, kuinua uchumi wa wananchi na kurasimisha shughuli za uchimbaji mdogo. 

Katika utekelezaji wa hatua hiyo, Serikali tayari imetenga eneo la Nyakafulu, Wilaya ya Mbogwe Mkoani Geita kwa wachimbaji wadogo na kutoa leseni 108 baada ya kufutwa kwa leseni zilizokuwa haziendelezwi ipasavyo.

Hatua hiyo imebainishwa bungeni leo Mei 26, 2026 na Naibu Waziri wa Madini, Mhe. Dkt. Steven Kiruswa kwa niaba ya Waziri wa Madini wakati akijibu maswali ya wabunge kuhusu maendeleo ya Sekta ya Madini.

Akijibu swali la Mbunge wa Mbogwe, Mhe. Fagason Nkingwa aliuliza kuwa ni lini Serikali itatenga maeneo kwa wachimbaji wadogo na kuwapatia leseni za uchimbaji, Dkt. Kiruswa amesema Serikali tayari imetenga eneo la Nyakafulu kwa ajili ya wachimbaji wadogo na kutoa jumla ya leseni 108 baada ya kufutwa kwa leseni ambazo hazikuwa zimeendelezwa.

Amesema kuwa, hatua hiyo inaakisi dhamira ya Serikali ya kuendelea kurasimisha na kukuza shughuli za uchimbaji mdogo nchini ili wananchi wengi zaidi waweze kushiriki katika uchumi wa madini kwa tija na manufaa mapana.

“Serikali kupitia Tume ya Madini inaendelea kufanya tathmini ya kisheria ya leseni 63 za utafiti ambazo hazijaendelezwa ipasavyo kwa lengo la kuzifuta pale inapobidi na kuyatenga baadhi ya maeneo hayo kwa wachimbaji wadogo,” amesema Dkt. Kiruswa.

Aidha, Dkt. Kiruswa ameeleza kuwa Serikali itaendelea kuchambua taarifa za jiosayansi ili kubaini maeneo yenye tija kwa wachimbaji wadogo, huku Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ikipewa jukumu la kufanya tafiti za kina kwenye maeneo yenye taarifa hafifu kabla ya kutengwa rasmi kwa shughuli za uchimbaji mdogo.

Katika hatua nyingine, Serikali imeeleza kuwa ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha uhakiki wa madai ya waliokuwa watumishi wa Mgodi wa Kiwira kabla ya kuanza kulipa madeni hayo.

Akijibu swali la Mbunge wa Kyela, Mhe. Baraka Mwamengo kuhusu lini Serikali itawalipa waliokuwa watumishi wa Mgodi wa Kiwira, Dkt. Kiruswa ameeleza madai hayo yalitokana na malalamiko ya mapunjo ya mafao kwa wafanyakazi waliokuwa wakihudumu mgodini hapo kabla ya ubinafsishaji.

Amefafanua  kuwa baada ya malalamiko kuwasilishwa na Chama cha Wafanyakazi Migodini na Ujenzi (TAMICO), Serikali ilifanya ukaguzi maalum kupitia Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali mwaka 2008 na baadaye kufanya uhakiki mwingine mwaka 2015.

Kwa mujibu wa uhakiki huo, madai halali ya wafanyakazi 893 yalibainika kuwa shilingi bilioni 1.024 tofauti na madai ya awali ya zaidi ya shilingi bilioni 47 yaliyokuwa yakidaiwa na wafanyakazi 1,687. Aidha, kulikuwepo na madeni ya wazabuni mbalimbali yaliyofanya jumla ya deni kufikia shilingi bilioni 1.52.

Dkt. Kiruswa amesema Serikali tayari imejumuisha madeni hayo kwenye orodha ya madeni ya Serikali na kwamba Wizara ya Madini inaendelea kushirikiana na Wizara ya Fedha kuhakikisha malipo yanafanyika baada ya kukamilika kwa uhakiki wa mwisho unaoendelea kwa sasa.

“Kwa sasa timu ya wataalamu inakamilisha taarifa ya mwisho ya uhakiki ili madeni hayo yaweze kulipwa na Serikali,” amesisitiza Dkt. Kiruswa.

Post a Comment

0 Comments