NA MWANDISHI WETU
Wakala
wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imezidi kujipambanua kama muhimili na
nguzo madhubuti katika kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa, kupitia mikakati yake
endelevu inayolenga kurasimisha shughuli za kiuchumi na kuhakikisha kuwa hakuna
Mtanzania anayeachwa nyuma katika upatikanaji wa huduma za sajili na leseni. Hayo
yamebainishwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa, wakati
akifungua kikao kazi cha wafanyakazi wa Wakala hiyo kilichofanyika mkoani
Morogoro tarehe 20 Juni 2026.
“Katika
mwaka wa fedha wa 2025/2026, BRELA imefanikiwa kuvuka malengo na kutekeleza
majukumu yake ya msingi kwa ufanisi mkubwa ikijikita katika kuboresha huduma
kwa wadau, kuimarisha mifumo ya kidijitali, na kupanua wigo wa urasimishaji
biashara nchini licha ya changamoto mbalimbali za kimazingira na kiuchumi
zilizojitokeza” Alisema Bw. Nyaisa
Aidha,
Kaimu Meneja wa Sehemu ya Mipango, Utafiti na Ubunifu wa BRELA, Bi. Alinda
Lema, alibainisha kuwa mafanikio hayo yamepatikana kupitia usimamizi thabiti wa
Mpango Mkakati wa miaka mitano wa 2021/22–2025/26. Katika kipindi cha kuanzia
Julai 2025 hadi Juni 2026, mpango huo umewezesha mazingira ya biashara nchini
kwa kuimarisha huduma za sajili na leseni, mifumo ya kiteknolojia, na usimamizi
wa utendaji kazi wa watumishi. Huku kukiwa na ongezeko la kasi ya urasimishaji
wa biashara, kuimarika kwa ulinzi wa haki miliki, na kurahisishwa kwa huduma
zote zinazowafikia wadau wa sekta binafsi na ya umma.
“Kampuni
zilizosajiliwa nchini zilipanda kutoka 18,541 katika mwaka wa fedha uliopita wa
2024/25 na kufikia kampuni 19,264 katika mwaka wa fedha wa 2025/26, ikiwa ni
ongezeko la asilimia 4 linaloakisi kuongezeka kwa imani ya wawekezaji wa ndani
na nje. Vilevile, upande wa urasimishaji wa biashara, usajili wa majina ya
biashara uliongezeka kutoka majina 31,123 hadi kufikia 35,362, ikiwa ni
ongezeko la asilimia 14” Alisema Bi. Lema
Kwa
upande wa sekta ya viwanda na miliki ubunifu nayo haikuachwa nyuma, kwani
ilionyesha ukuaji unaochochea azma ya Tanzania kuwa nchi ya viwanda na uchumi
wa kati. Bi. Lema alifafanua kuwa utoaji wa leseni za viwanda uliongezeka kwa
asilimia 50, kutoka leseni 435 hadi leseni 651 katika kipindi cha mwaka mmoja tu.
Hali kadhalika, utoaji wa Hataza (Patents) kwa ajili ya kulinda wavumbuzi wa
ndani ulishuhudia mapinduzi kwa kuongezeka kutoka hataza 30 hadi 61, ambalo ni ongezeko
la asilimia 103, wakati usajili wa alama za biashara na huduma (Trade and
Service marks) ukiongezeka kwa asilimia 10 kutoka sajili 3,148 hadi kufikia
3,455, hatua inayolinda alama na ubunifu wa wafanyabiashara sokoni.
BRELA ilitekeleza zoezi la kaguzi elimishi kwa
upande wa leseni katika soko kuu la kimkakati la Kariakoo jijini Dar es Salaam.
Ukaguzi huu haukulenga kuadhibu, bali kuweka mazingira rafiki ya uendeshaji
biashara na uwekezaji kwa kutoa elimu ya uzingatiaji wa sheria za nchi. Katika
hatua nyingine ya uwazi na udhibiti wa mifumo ya kifedha, Wakala ilifanikiwa
kufanya ukaguzi wa kina wa taarifa za wamiliki manufaa (Beneficial Ownership)
katika mkoa wa Arusha, hatua iliyosaidia kuongeza uelewa na kupunguza makosa
yaliyokuwa yanajitokeza katika mfumo wa usajili wa kampuni.
Mkakati
huu wa ukaguzi ulienda sambamba na utoaji endelevu wa elimu kwa umma kuanzia
Julai 2025 hadi Juni 2026, ambapo BRELA ilitumia mbinu mbalimbali za kisasa
kuwafikia wananchi. Elimu kuhusu urasimishaji wa biashara, umuhimu wa leseni,
na faida za kulinda miliki ubunifu ilitolewa kupitia mafunzo ya ana kwa ana,
semina maalum, maonesho ya kibiashara, vipindi vya redio na televisheni, pamoja
na kushiriki katika kliniki za biashara. Ushirikiano wa karibu na vyama vya
wafanyabiashara nchini pia ulichangia kwa kiasi kikubwa kurahisisha ufikishaji
wa ujumbe na kubadili mtazamo wa jamii kuelekea mifumo rasmi.
Sambamba
na hayo, BRELA imepiga hatua baada ya kuzindua rasmi mfumo mpya na wa kisasa
unaojulikana kama BRELA Online Services
(BOS). Mfumo huu mpya ni mapinduzi kwani unajumuisha na kuunganisha huduma zote
zilizokuwa zinatolewa kwa wateja kupitia mifumo miwili tofauti hapo awali,
yaani Online Registrations System
(ORS) na Tanzania National Business
Portal (TNBP). Kupitia mfumo huu wa BOS, mteja sasa anaweza kupata huduma
zote za usajili wa kampuni, majina ya biashara, alama za biashara na huduma, hataza,
pamoja na leseni kupitia huo mmoja.
Akiangazia
mipango na mustakabali wa Wakala hiyo kwa siku zijazo, Bi. Lema alisema kuwa
katika kipindi kipya cha mwaka wa fedha kuanzia Julai 2026 hadi Juni 2027,
BRELA imejipanga kuongeza takribani asilimia 17 ya urasimishaji biashara na
kulinda ubunifu nchini. Mkakati huu utatekelezwa kwa kuzingatia misingi mikuu
ya dira ya Taifa ya maendeleo 2050, Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka
Mitano (FYDP IV), pamoja na Mpango Mkakati mpya wa miaka mitano wa Wakala wa
mwaka 2026/27–2030/31. Katika kufikia lengo hili, Wakala imejipanga kusajili
kampuni mpya 24,103, majina ya biashara 40,460, alama za biashara na huduma
4,500, na hataza 40, huku ikipanga kutoa leseni za biashara 29,533 na leseni za
viwanda 638.
Bi. Lema alisisitiza kuwa ili kuhakikisha azma hiyo inafikiwa na mazingira ya uwekezaji yanazidi kuwa ya ushindani kikanda na kimataifa, BRELA itafanya mapitio ya sheria na kanuni zote za sajili na leseni. Mapitio haya yatafanyika ili kuhakikisha sheria hizo zinaendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia duniani, kukidhi mahitaji ya sasa ya wadau, na kuendana na misingi ya uchumi wa kisasa, na hivyo kuifanya Tanzania kuwa kitovu bora zaidi cha uwekezaji na ukuaji wa biashara barani Afrika.


0 Comments