MBETO: CHADEMA ILIWASALITI WATANZANIA ILIPOSUSIA UCHAGUZI MKUU 2025


Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kinadaiwa kuwasaliti waTanzania kwa kususia uchaguzi mkuu uliopita 2025 jambo linalofanya michango ya maoni yao katika mjadala wa Bajeti Kuu ya Serikali 2025/2026 unaoendelea, Dodoma kukosekana.

Akizungumza na wanahabari mjini Unguja, Katibu wa Kamati Maalum NEC Zanzibar Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis alisema, badala yake wamekuwa wakisemea vichochoroni na kugombana na polisi na kuwa wanasiasa wa matukio na visasi.

Mbeto alisema Bunge ni chombo cha kisheria ambako mijadala na hoja zinazowahusu wananchi hujadiliwa lakini wao hawapo baada ya kuwasaliti wananchi kwa kususia uchaguzi mkuu uliopita na hivi sasa wamegeuka kuwa wanaharakati.

Alisema mwenezi huyo kuwa wananchi wanakosa ladha ya mijadala bungeni iliyokuwa inaibuliwa na wabunge wao mahiri wakiwemo kina Tundu Lissu, Zitto Kabwe, Joseph Mbilinyi 'Sugu', Kafulila na wengine.

"Tatizo la Chadema wametoka kwenye kufanya siasa wamekuwa wana harakati, mara oooh, no reform no nini sijui, mara Mwanza kuna Ziwa lakini hakuna maji na kila siku kulaumu vyombo vya ulinzi na usalama wakiwemo polisi" alisema Mbeto.

Mwenezi huyo alieleza kuwa chama hicho kimepoteza ushawishi kwa umma na hata wanaposema kura ziliibwa na kuhoji ushindi wa zaidi ya asilima 95 wa Rais Samia hawana hoja kwani wao ndio chama kikuu cha ushindani na hakikushiriki walitegemea nini.

Mbeto alibainisha kuwa CCM haina muda wa mipasho bali kuwatumikia wananchi na hakikatai kukosolewa ili mradi iwe kwa hoja na katika vyombo vya kisheria.

Mwenezi huyo anawakumbusha kuwa kupitia hoja za wabunge wao kwa mara ya kwanza katika historia ya Jamhuri ya Muungano, Waziri Mkuu alistaafu, mara kadhaa Baraza la Mawaziri lilifanyiwa mabadiliko lakini kwa kuwa wameamua kuwa wana harakati wananchi wanakosa haki yao ya kusikia hoja na maoni mbadala katika mambo ya msingi ya maendeleo yao.

"Serikali ni sikivu ndio maana ilifanya mabadiliko kadhaa kwenye miswada iliyokuwa inawasilishwa, Bungeni kutokana na hoja za wabunge wao" alisema Mbeto  na kuongeza kuwa wabunge hao wa upinzani waliibua madudu mengi ambayo serikali iliyafanyiakazi.

Post a Comment

0 Comments