RAIS DKT. MWINYI AKUTANA NA JAJI MKUU MASAJU, ASISITIZA MAGEUZI YA KIDIJITALI MAHAKAMANI




NA MWANDISHI WETU

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) katika utendaji wa Mahakama ni eneo muhimu linalopaswa kupewa kipaumbele ili kuharakisha upatikanaji wa haki na kuongeza ufanisi.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 22 Juni 2026, alipokutana na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Jaji George Masaju, aliyefika Ikulu Zanzibar kwa ajili ya kujitambulisha.

Amesema Mahakama ya Zanzibar ina fursa ya kujifunza kutokana na mafanikio yaliyofikiwa na Mahakama ya Tanzania katika matumizi ya Tehama, kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati na kupunguza gharama za kiutendaji.

Rais Dkt. Mwinyi amepongeza ushirikiano uliopo baina ya Mahakama ya Zanzibar na Mahakama ya Tanzania na kusisitiza umuhimu wa kuuendeleza ili kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya pamoja kwa manufaa ya wananchi.

Aidha, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweka mkazo katika matumizi ya Tehama na uimarishaji wa miundombinu ya Mahakama katika ngazi zote, ili wananchi wapate huduma za haki kwa wakati, katika mazingira bora na karibu na maeneo wanayoishi.

Akizungumzia ujenzi wa miundombinu ya Mahakama, Rais Dkt. Mwinyi amesema ujenzi wa jengo la Mahakama ya Rufani Pemba ni hatua muhimu itakayowezesha majaji kutekeleza majukumu yao katika mazingira bora na kuimarisha huduma za kimahakama kisiwani humo.

Kwa upande wake, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Jaji George Masaju, amepongeza ushirikiano unaotolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Mahakama ya Zanzibar. Aidha, amesema uamuzi wa kujenga Mahakama ya Rufani Pemba ni wa busara na kuahidi kusimamia ujenzi huo ili ukamilike kwa wakati, kwa lengo la kuwapatia wananchi huduma bora za haki na kuwapunguzia gharama za kufuatilia mashauri yao.

Post a Comment

0 Comments