TIRA YAJIPANGA KUENDELEZA MAGEUZI YA HUDUMA ZA BIMA KUFUATIA MAELEKEZO YA WAZIRI RIDHIWANI KIKWETE





NA MWANDISHI WETU

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), imeshiriki katika ufunguzi rasmi wa Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2026 yanayofanyika katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma, ambapo mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Jakaya Kikwete (Mb).

Akizungumza wakati wa ufunguzi huo, Mhe. Kikwete alisema kuwa Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma ni jukwaa muhimu linalowapa wananchi fursa ya kufahamu huduma mbalimbali zinazotolewa na Serikali pamoja na namna ya kuzifikia kwa urahisi. Aidha, alisisitiza umuhimu wa taasisi za umma kuendelea kuboresha huduma, kuimarisha matumizi ya teknolojia za kidijiti, kuongeza uwajibikaji na kuhakikisha wananchi wanashirikishwa kikamilifu katika utoaji wa huduma.

Akiiwakilisha TIRA katika ufunguzi huo, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Bw. Nakaunda Baraka alisema maelekezo yaliyotolewa na Mhe. Waziri yanaendana moja kwa moja na juhudi zinazoendelea kufanywa na TIRA katika kuboresha usimamizi wa sekta ya bima na kuongeza upatikanaji wa huduma za bima kwa wananchi.

Alieleza kuwa TIRA imeendelea kuwekeza katika matumizi ya mifumo ya kidijiti na ubunifu ikiwemo TIRAMIS, IRIS, ORS na TSS Billing inayorahisisha utoaji wa huduma za bima, kuongeza uwazi katika usimamizi wa sekta na kuwafikia wananchi wengi zaidi kidijitali.

Maadhimisho haya yanatoa fursa kwa TIRA kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa bima, huduma zinazopatikana katika sekta ya bima pamoja na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali kupitia TIRA katika kuimarisha ulinzi wa watumiaji wa huduma za bima.

Maono ya Serikali ya kuwa na utumishi wa umma wenye tija, unaowajibika na unaotumia teknolojia yanaakisiwa katika hatua ambazo TIRA imekuwa ikizichukua za kuimarisha mifumo ya utoaji huduma, kusogeza huduma karibu na wananchi na kuchochea ubunifu wa bidhaa za bima zinazokidhi mahitaji ya Watanzania.

Kupitia maadhimisho haya, TIRA itaendelea kutoa elimu kwa wananchi, kusikiliza maoni yao na kuwaelekeza kuhusu fursa mbalimbali zinazopatikana katika sekta ya bima, ikiwa ni sehemu ya mchango wake katika kuunga mkono azma ya Serikali ya kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Post a Comment

0 Comments