NA MWANDISHI WETU
Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu
wa Petroli (PURA) imesisitiza umuhimu wa kuendelea kuvutia uwekezaji,
kuimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali pamoja na kutumia ipasavyo fursa
zilizopo katika sekta ya mafuta na gesi asilia ili kuongeza mchango wake katika
maendeleo ya uchumi wa Taifa.
Akizungumza katika Kongamano la
Siku ya Nishati (Energy Day) linaloendelea katika Ukumbi wa Mwandoro, Viwanja
vya Mwalimu Julius Nyerere – Sabasaba, jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa
PURA, Mhandisi Charles Sangweni, alisema usimamizi na udhibiti madhubuti wa
shughuli za mkondo wa juu wa petroli ni msingi muhimu wa kuhakikisha rasilimali
za mafuta na gesi zinatumika kwa manufaa ya Taifa.
Mhandisi Sangweni alieleza kuwa
sekta ya mafuta na gesi asilia ina nafasi kubwa katika kuchangia ukuaji wa
uchumi wa Taifa kupitia uwekezaji, uendelezaji wa rasilimali na kuongeza
thamani ya shughuli za kiuchumi zinazotokana na sekta hiyo.
Aliongeza kuwa ushirikiano kati ya
Serikali, wawekezaji na wadau wengine wa sekta hiyo utaendelea kuwa nguzo
muhimu katika kufanikisha maendeleo endelevu ya sekta ya mafuta na gesi nchini.
Kongamano hilo limewakutanisha viongozi, wataalamu, wawekezaji, washirika wa maendeleo na wadau wengine wa sekta ya nishati kujadili mwelekeo wa sekta, fursa za uwekezaji, ubunifu na matumizi ya teknolojia kwa ajili ya kuharakisha maendeleo ya Tanzania.

0 Comments