Wizara ya Nishati imesisitiza
umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, taasisi zilizo chini ya wizara, sekta
binafsi na wadau mbalimbali katika kuharakisha maendeleo ya sekta ya nishati na
kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya uhakika kwa maendeleo ya kiuchumi na
kijamii nchini.
Akizungumza katika Kongamano la
Siku ya Nishati (Energy Day) linaloendelea katika Ukumbi wa Mwandoro, Viwanja
vya Mwalimu Julius Nyerere – Sabasaba, jijini Dar es Salaam, Mhandisi Mkuu wa
Nishati, Bw. Christopher Nyondo, alisema Wizara ya Nishati inaendelea
kutekeleza majukumu yake kwa kushirikiana na taasisi zilizo chini yake katika
kusimamia maendeleo ya sekta hiyo.
Bw. Nyondo alieleza kuwa wizara
inaendelea kuratibu shughuli za sekta ya nishati, kusimamia utekelezaji wa
miradi mbalimbali pamoja na kuimarisha upatikanaji wa nishati kwa lengo la
kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kuboresha ustawi wa wananchi.
Aliongeza kuwa ushirikiano wa
karibu kati ya Serikali, taasisi za nishati, sekta binafsi na wadau wengine ni
msingi muhimu wa kufanikisha malengo ya maendeleo ya sekta hiyo na kuongeza
mchango wake katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Kongamano hilo limewakutanisha
wadau mbalimbali wa sekta ya nishati kujadili fursa za uwekezaji, ubunifu na
maendeleo yanayoendelea katika sekta hiyo nchini.

0 Comments