Na Mwandishi Wetu, Dodoma
DODOMA — Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Kati, kwa kushirikiana na Ofisi ya Elimu Mkoa na Wilaya ya Dodoma, umewapa mafunzo walimu wa mazingira wa Jiji la Dodoma kuhusu dhana, sababu na athari za mabadiliko ya tabianchi katika mazingira ya shule.
Mafunzo hayo yaliyofanyika Julai 29 na 30, 2026 katika Shule ya Msingi Mtemi Mazengo, yalilenga kuwawezesha walimu hao kuwa mabalozi wa elimu ya mazingira kwa wanafunzi na jamii zinazowazunguka.
Akitoa mafunzo hayo, Mhifadhi wa TFS, Zureikha Abubakary Kachwamba, aliwataka walimu kutumia ubunifu katika kuwajengea wanafunzi uelewa kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira ili wawe chachu ya mabadiliko katika jamii.
Mgeni rasmi, Afisa Elimu wa Mkoa wa Dodoma, Mwalimu Kiduma Mageni, aliipongeza TFS kwa kuendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali katika kutoa elimu ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Alisema elimu hiyo ni muhimu katika kujenga kizazi chenye uelewa wa uhifadhi wa mazingira na kuhimiza walimu kuitumia kuwafundisha wanafunzi pamoja na kuhamasisha shughuli za upandaji miti mashuleni na katika maeneo wanayoishi.
Aidha, aliwataka walimu kuhamasisha ufugaji wa nyuki kama njia mbadala ya kuongeza kipato huku ukiunga mkono juhudi za uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.


0 Comments