NA MWANDISHI WETU
Waziri wa maliasili na utalii Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) leo tarehe 10 julai, 2026 amekutana na bodi ya wakurugenzi mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro katika ofisi za mamlaka hiyo zilizopo Karatu mkoani Arusha na kusisitiza umuhimu wa bodi hiyo kufuatilia kwa karibu shughuli zote za utendaji ili kuanza mwaka mpya wa fedha 2026/2027 kwa kasi na ufanisi.
Mhe. Kijaji amesema kuwa bajeti ya mwaka mpya wa fedha inaanza na utekelezaji wa dira ya taifa ya maendeleo ya mwaka 2050 hivyo vikao vyake na bodi za taasisi zilizopo chini ya wizara vina lengo la kuanza utekelezaji wa dira, bajeti na ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa pamoja.
Ameitaka bodi hiyo kuongeza nguvu katika kuimarisha uhifadhi, kutangaza utalii na kusimamia maendeleo ya jamii na kusisitiza kuwa jitihada hizo ziendane na kasi ya kukamilisha miundombinu wezeshi ikiwemo barabara kuu ya Loduare hadi Golini, kuimarisha mawasiliano ndani ya eneo lote la hifadhi, kukamilisha mradi wa fensi ya umeme ili kupunguza migongano kati ya wanyamapori na wananchi, kudhibiti ujangili na kuendelea kuimarisha mahusiano ya hifadhi na wananchi wanaoizunguka.
“Tulinde uhifadhi wa Ikolojia ya Ngorongoro kwa wivu mkubwa, tuendelee kubuni mazao mapya ya utalii na kuyatangaza, tujipange kikamilifu kuhakikisha Ngorongoro kama premium destination inawafikia na kuwashawishi wageni watakaohudhuria matukio ya AFCON, mkutano wa umoja wa Mabunge duniani, tuzo za dunia za utalii na shindano la Miss world ambapo matukio yote yatafanyika Tanzania kati ya mwezi oktoba 2026 na Julai mwaka 2027” amesisitiza Dkt. Kijaji.
Katibu wa Bodi, ambae ni kamishna wa Uhifadhi Ngorongoro Abdul-Razaq Badru amemueleza Mhe. waziri kuwa, Ngorongoro imepiga hatua ya kimageuzi kwenye mifumo ya kidijitali (ICT Transformation), uhifadhi endelevu kwa kuimarisha doria za kisasa, kuboresha miundombinu hasa barabara ya tabaka gumu kutoka geti la loduare hadi Seneto (km 29.5) kwa gharama ya TZS 80.3 bilioni
Badru ameongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2025/26 eneo la Ngorongoro idadi ya watalii ilifikia 1,061,620 na fedha shilingi 269.5 Bilioni zilikusanywa. Ngorongoro imeendelea na jitihada za kulinda hadhi tatu za kimataifa kutoka UNESCO ambazo ni Urithi wa Dunia (World Heritage Site), Hifadhi ya Biosphere (Man and Biosphere Reserve), na Geopark ya Dunia (Ngorongoro-Lengai Global Geopark) ili ziendelee kuinufaisha nchi yetu.
Kwa upande wake makamu mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi Ngorongoro Dkt. Harriet Mtae amemueleza Mhe waziri kuwa, katika kipindi cha miezi sita (06) iliyopita bodi ya Ngorongoro imetekeleza majukumu kwa kuzingatia sheria, kanuni pamoja na maelekezo ya Serikali ili kuhakikisha Mamlaka inatekeleza kikamilifu dhamana yake ya kuhifadhi maliasili za Wanyamapori, malikale na urithi wa dunia, kuendeleza utalii endelevu na kuboresha shughuli za maendeleo ya jamii.

0 Comments