NA MWANDISHI WETU, LONGIDO
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Ndugu Nassoro Shemzingwa, leo Agosti 12, 2026, amezikabidhi bendera timu za Halmashauri hiyo zinazokwenda kushiriki Mashindano ya Shirikisho la Michezo kwa Serikali za Mitaa (SHIMISEMITA), yanayotarajiwa kufanyika kuanzia Agosti 15 hadi 29, 2026, jijini Mbeya.
Halmashauri ya Wilaya ya Longido inawakilishwa na timu nne katika mashindano hayo, ambazo ni Mpira wa Miguu (Football), Netball, Volleyball na Basketball.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano hayo iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri, J.K. Nyerere, Ndugu Shemzingwa amewataka wachezaji kwenda kushiriki mashindano hayo kwa ari, umoja na kuzingatia nidhamu.
“Endeleeni na maandalizi, mkashiriki mkiwa na ari. Nendeni mkashiriki mkiwa na umoja. Nasistiza, mnapokwenda huko muwe na umoja, mzingatie sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma mkiwa huko. Twendeni tukashiriki kifua mbele, tusiende kinyonge,” amesema Ndugu Shemzingwa.
Ndugu Shemzingwa ametumia fursa hiyo kuwapongeza wachezaji wote wanaokwenda kuiwakilisha Halmashauri ya Wilaya ya Longido katika mashindano hayo, akiwapongeza pia kwa jitihada zao binafsi katika kufanya mazoezi na kujiandaa kwa ajili ya mashindano.
Amesema kuwa pamoja na kuwa ni watumishi wa umma, wanahimizwa kushiriki katika michezo inayowaunganisha pamoja, huku michezo ikiwa na mchango mkubwa katika kupambana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
Aidha, ameahidi kuendelea kuwapa ushirikiano ili kuhakikisha wanafikia malengo yaliyowekwa na kushiriki mashindano hayo kwa ufanisi.



0 Comments