Na WMA - NYAKABINDI, SIMIYU
Wakala wa Vipimo (WMA) umefanikiwa kupata nafasi ya Mshindi wa Pili katika kundi la Taasisi za Umma kwenye Kilele cha Maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi (Nane Nane) Kanda ya Ziwa Mashariki.
Maonesho hayo yaliyohusisha mikoa ya Mara, Simiyu na Shinyanga yalifanyika katika Viwanja vya Nyakabindi, Mkoa wa Simiyu na kumalizika kwa ushindi huo mnono kwa WMA.
Mgeni Rasmi katika Hafla ya kilele cha maonesho hayo alikuwa ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo ambaye ndiye aliwakabidhi WMA cheti na kikombe cha ushindi wa pili sambamba na washindi wengine.
Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo, Meneja wa WMA Mkoa wa Simiyu, Bi. Happy Titi alisema ushindi huo ni matunda ya jitihada za WMA katika kutoa elimu kwa wakulima na wafanyabiashara kuhusu umuhimu wa kutumia vipimo sahihi.
“Tunamshukuru Mungu na tunampongeza Afisa Mtendaji Mkuu na wafanyakazi wote. Ushindi huu unatupa nguvu zaidi ya kuendelea kuelimisha jamii yetu ya Kanda ya Ziwa Mashariki kuhusu vipimo sahihi ili kuongeza tija na kuepuka hasara katika biashara,” alisema Bi. Titi.
Katika kipindi chote cha maonesho, Wataalamu wa WMA walikuwa wakitoa elimu kuhusu matumizi ya vipimo sahihi katika mazao ya kilimo na mifugo pamoja na umuhimu wa kutumia mizani iliyohakikiwa.
Bi. Titi amewashukuru wananchi wote wa mikoa mitatu waliofika katika banda la WMA na kuahidi kuendelea kutoa huduma bora zaidi.

.jpeg)

0 Comments