CCM: HEKO RAIS DK MWINYI KUPANDISHA MISHAHARA ZANZIBAR

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

Chama Cha Mapinduzi kimempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi kwa kutekeleza ahadi ya Serikali yake kupandisha Mishahara ya Wafanyakazi.

Pia CCM kimeitaja hatua hiyo ni utekelezaji unaothibitisha azma ya SMZ ya kupandisha Mishahara kutokana na nia safi alionayo Rais huyo.

Pongezi hizo zimetolewa na Katibu wa Kamati  Maalum  ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis huko  Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui kisiwani Unguja.

Mbeto alisema siku zote ahadi  huwa  zaidi ya deni ,na pale ahadi  inapotelelezwa,  huthibitisha  uungwana wa mtu alieahidi na kutimiza ahadi yake .

Alisema kitendo cha Serikali ya Awamu ya Nane kupandisha Mshahara kwa kima cha chini toka laki 3 hadi 5 kwa Mwezi, kinapaswa kuuungwa mkono na kupongezwa .

"Chama Cha Mapinduzi kwa dhati kabisa kinampongeza Rais Dk Mwinyi kwa hatua ya  Serikali yake kupandisha kima Cha chini cha Mishahara. Pia nyongeza hiyo ya Mishahara imefanyika kwa Wafanyakazi wa  madaraja mengine " Alisema Mbeto.

Katibu huyo Mwenezi alisema Mei Mosi Mwaka  huu katika Maadhimisho ya siku ya Wafanyakazi Duniani, Rais Dk Mwinyi aliahidi kuwa serikali yake itaongeza mishahara kwa wafanyakazi wa SMZ.

Sherehe za Mei Mosi zilifanyika huko Dole Kizimbani Wilaya ya Magharibi A, Mkoa wa Magharibi Kisiwani Unguja.

"Waswahili husema Ada ya mja hunena uungwana ni vitendo. Ahadi ya Rais Dk Mwinyi imetimia kwa Wafanyakazi wote wa Serikali. Yote yalioahidiwa yataendelea kutekelezwa "Alisisitiza.

Aidha, Katibu huyo Mwenezi aliwataka Viongozi dhamana wa Serikali katika upandishaji viwango vya Mishahara katika Wizara,Taasisi, Idara na kwenye  Vitengo vya SMZ , kusitokee urasimu utakaoleta manung'uniko katika upandishaji  Mishahara mipya.

"Kazi ya upandishaji mishahsra kwa madaraja  yote itaanza rasmi Mwezi huu .Itapendeza  endapo hakutojitokeza malalamiko  toka kwa Mfanyakazi wa daraja lolote "Alishauri Mbeto.

Post a Comment

0 Comments