DC GONDWE AWATAKA WAKUU WA VIKOSI VYA USALAMA BABARANI DAR KUWACHUKULIA HATUA MADEREVA WASIOFUATA SHERIA



Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam Godwin Gondwe (kulia) akitoa vyeti kwa wadau walioshiriki katika maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani kwa Kanda Maalum ya Dar es Salaam

NA ABRAHAM NTAMBARA

MKUU wa Wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam Godwin Gondwe amewataka wakuu wa vikosi vya Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Kanda Maalum ya Dar es Salaam kuwachukulia hatua kali madereva wasiofuata sheria.

Gondwe ametoa kauli hiyo leo katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam wakati akifunga maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani kwa Kanda Maalum ya Dar es Salaam.

“Lengo ni ili kunusuru vifo, majeraha na ulemavu kwa wananchi,” amesema Gondwe.

Hata hivyo amewataka wananchi wasiwe mashabiki wa mwendo kasi wanapokuwa kwenye vyombo vya moto na badala yake watoe taarifa kuhusu madereva wanaoendesha kwa kasi na kutofuata sheria za barabarani.

Akizungumzia maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani kwa Kanda Maalum ya Dar es Salaam amelipongeza Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani kwa kupeleka askari trafiki kutoa elimu ya usalama barabarani mashuleni, na maeneo mbalimbali ikiwemo katika vijiwe vya bodaboda.

Hata hivyo Gondwe amesema ili kufanikisha mapambano dhidi ya ajali za barabarani ni lazima kila mtu kutimiza wajibu wake.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Barabarani Kanda Maalumu ya Dar es Salam ZTO Abduli Isango amesema katika kipindi cha maadhimisho hayo Jehi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani kilitoa elimu ya usalama barabarani katika shule 14 za jijini Dar es Salaam.

“Tulitoa pia elimu kwa madareva bodaboda na madereva bodaboda zaidi ya 2,000 wamepata elimu hiyo. Madeva wa magari pia zaidi ya 2,000 wamepata elimu. Vile vile tumetoa elimu kwa askari wa usalama barabarani,” amesema ZTO Isango.

Naye Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ajali kutoka Hospitali ya Muhimbili Kitengo cha Mifupa (MOI) Dkt. Joseph Mwanga amesema kuwa wagonjwa wanaowapokea kwa kiasi kukibwa zaidi ya asilimia 50 ni waajali za pikipiki.

“Wanakuwa wameumia sana kuanzia kwenye mfumo wa ubongo, miguu na kifuani. Wiki hii pekee tumepokea majeruhi 42 na zaidi ya 30 wanahitaji upasuaji wa mifupa,” amesema Dkt. Mwanga.

Dkt. Mwanga amesema mgonjwa akishakuwa katika hali hiyo anakuwa dhaifu na hawezi kurudi katika hali yake ya kawaida na kuweza kufanya shuguli zake za uzalishaji hali ambayo inaathiri familia kwani anakuwa mzigo wa kuhitaji msaada wa kuhudumiwa.

HABARI KATIKA PICHA


 

Post a Comment

0 Comments