NA MWANDISHI WETU
CHAMA cha ACT Wazalendo kimeiomba Serikali kuwachukulia hatua viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Makamu Mwenyekiti Bara, Stephen Wasira, na Naibu Katibu wa Habari na Uenezi wa CCM-Zanzibar, Hamis Mbeto, kwa kupotosha umma kuhusu kuzuiliwa kwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Othman Masoud Othman nchini Angola.
Ombi hilo limetolewa leo Machi 16, 2025 na Mwenyekiti wa Chama hicho ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar akizungumza na waandishi wa habari Makao Makuu ya Chama Magomeni jijini Dar es Salaam kuhusu tukio la viongozi wa chama hicho kuzuiliwa nchini Angola waalipkuwa wamekwenda kuhudhuria mkutano wa kidemokrasia.
“Pmoja na taarifa zote zilizotolewa kuhusu tukio hili, watu wanapotosha juu ya jambo hili tena wanaofanya upotoshaji huu ni viongozi wa juu wa CCM Makamu Mwenyekiti Wasira na Naibu Katibu wa Habari na Uenezi wa CCM-Zanzibar, Hamis Mbeto. Niseme wito wangu kwamba hasa kwa haya ambayo yamepotoshwa na watu ambao ni waandamizi wa Chama cha Mapinduzi, naiomba sana Serikali na natoa wito serikalini kama Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo kwamba Serikali iwachukulie hatua viongozi hao, kwa sababu upotoshaji wao umeipaka matope Serikali," amesema Othman na kuongeza.
"Upotoshaji wao umewafadhaisha wananchi kwa kiasi kikubwa, wamefanya vitu kwa namna ambayo haiendani na nafasi zao, huo ndiyo wito wetu kama ACT,”.
Othman amesema kuwa kama kiongozi wa Serikali kabla ya kwenda nje ya nchi alifuata taratibu zote zinazotakiwa ikiwemo kuomba ruhusa kwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dkt. Hussein Ally Mwinyi na aliruhusiwa kwa barua ya maandishi.
Machi 14, akizungumza Tunduma mkoani Songwe, Wassira alisema: "Leo nimesoma viongozi walikuwa wanaenda Angola lakini wamenyang'anywa paspoti huko ni Angola sio hapa, hapa hatuja wanyang'anya paspoti na hata ikimaliza muda wake tunawapa, ili waende wanakotaka alafu warudi salama.
“Wamelalamika kwa nini Serikali imekaa kimya kwani sisi tunasimamia Airpoti ya Angola? Airpoti ya Angola inasimamiwa na watu wa Angola, na pia huenda walikuwa na jambo lao ambalo wanalilitilia shaka wangeuawa tungesema kwa nini wamewaonea watu wasiokuwa na hatia," amesema Wassira.
Kwa upande wake Kiongozi wa Chama Dorothy Semu ameitaka Serikali kutoka hadaharani kueleza sababu zilizofanya wazuiliwe nchini Angola kwani hadi leo hawajui sababu na Serikali ya Tanzania haijatoa kauli yoyote.
Sambamba na hilo Semu ameitaka Serikali kumuita Balozi wa Angola nchini kueleza sababu za tukio hilo ambapo pia ameshauri Umoja wa Afrika (AU)kumpa uenyekiti wa AU Rais mwingine kwani Rais wa Angola ambaye ndiyo mwenyekiti wa sasa hatoshi.
Viongozi wa ACT Wazalendo walizuiwa kuingia nchini Angola kushiriki katika mazungumzo ya Jukwaa la Demokrasia Afrika (PAD), yaliandaliwa na Taasisi ya The Brenthurst Foundation.

0 Comments