NA MWANDISHI WETU
MSEMAJI Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa amesema Bandari Kavu ya Kwala iliyopo wilayani Kibaha mkoani Pwani ina uwezo wa kuhudumia kontena 823 kwa siku.
Msigwa amebeinisha hayo leo Machi 16, 2025 akizungumza na waandishi wa habari katika eneo la bandari hiyo ambapo amebainisha kuwa ina uwezo wa kuhudumia kontena 300,000 kwa mwaka na kwamba ni mara tatu ya Bandari ya Dar es Salaam.
Ameeleza kuwa bandari hiyo na zingine zinazojengwa Mwanza, Isaka, Dodoma, Tabora na mipakani mwa nchi za Burundi, Rwanda, Congo DR zitapunguza msongamano wa shehena Bandari ya Dar es Salaam.
Katika hatua nyingine akizungumzia utata unaoendelea kuhusu mchezo wa Simba dhidi ya Yanga ulioahirishwa na Bodi ya Ligi Machi 8, 2025 kutokana na Simba kuzuiliwa kufanya mazoezi, amesema suala hilo linabaki kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) na vyombo vyake, kwani serikali haitaki kutia neno.
Msigwa amebainisha hayo wakati akijibu swali la mwandishi wa habari lililohoji ni upi uamuzi wa serikali kuhusu kuahirishwa kwa mchezo huo.
Hivyo amesema ikitokea TFF wamepeleka suala hilo serikalini basi kwa pamoja watajadili ila kwa sasa serikali haina neno kwa suala lipo kwenye mamlaka zinazohusika.
“Mengine nani alikuwa sahihi na hakuwa sahihi mkawaulize TFF, wao ndio watakuwa na majibu ya jambo hili, lakini sisi kwa sasa serikalini bado tunaona jambo linaweza likatatuliwa na Shirikisho la Kandanda Tanzania (TFF) na wadau wake," amesema Msigwa.
Kuhusu Mechi ya robo fainali Kombe la Shirikisho Afrika kati ya Simba na Al-Masry, huenda ikapigwa uwanja wa Benjamini Mkapa mara baada ya maboresho yaliyoagizwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kukamilika.
“Uwanja upo tayari, wakaguzi wanakuja tarehe 20, sisi tumewaomba waje hata kabla ya hapo watakuja wauone uwanja uko tayari, pitch nzuri kabisa,” amesema Msigwa.

0 Comments