SERIKALI YA AWAMU YA SITA YAITAKA JAMII KUFICHUA 'KAUSHA DAMU' ILI KUIONDOA KWENYE MATATIZO


*#KAZIINAONGEA*

Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia Wizara ya Fedha imeitaka jamii hususani wakazi wa Wilaya ya Tarime Mkoani Mara, kutoa taarifa kwa Mamlaka husika inapobainika uwepo wa mtoa huduma ndogo za fedha asiyesajiliwa na anayetoa huduma kinyume cha Sheria.

Kiongozi wa Timu ya Wataalamu wa Elimu ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Salim Khalfan Kimaro ametoa kauli hiyo wakati wa zoezi la kutoa elimu ya fedha katika maeneo ya Manga, Sirari, Matombo, Nyamwaga, Ganyange na Gorong’a, yaliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Tarime Mkoani Mara.
 
Bw. Kimaro amesema kuwa uwepo wa watoa huduma ya fedha wasio sahihi wanachangia kwa kiasi kikubwa kufifisha maendeleo ya wananchi jambo ambalo Serikali haiwezi kulifumbia macho.
 
“Tumekuja kutoa elimu, tunafanya kwa jitihada kubwa kuhakikisha kwanza wananchi wanauelewa wa masuala ya fedha, wanatambua haki zao wakati wa kupata huduma za fedha na pia kuwa na uwezo wa kutambua huduma iliyo sahihi na isiyo sahihi ili waweze kuchukua hatua ikiwemo kupeleka taarifa katika Mamlaka husika pale inapobainika kuna changamoto ya watoa huduma hao”, amesema Bw. Kimaro.
 
Aidha, aliwataka wananchi kusimamia fedha zao na kuepuka kufanya sherehe au ngoma na mambo mengine yasiyokuwa ya maendeleo wanapopata fedha zinazotokana na shughuli zao halali za kiuchumu na badala yake wajiwekee akiba maeneo yenye tija kama vile Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja na Hati fungani za Serikali.
 
Kimaro amesema kuwa Utafiti wa FinScope wa mwaka 2023 nchini, unaeleza kuwa ni asilimia 53.5 tu ya nguvukazi ndiyo waliotumia huduma rasmi za fedha na hivyo kubaki na kundi kubwa la Watanzania ambao hawafaidiki na huduma hizo na hivyo kukosa fursa za kuboresha maisha yao kupitia shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Amesema kuwa Programu ya Elimu ya Fedha kwa umma ilianza Mei, 2024, na hadi sasa mikoa 15 imefikiwa na uelekeo ni Mkoa wa Mwanza ambao anaamini watu wengi zaidi watajitokeza kupata elimu ya fedha kwa manufaa ya maisha yao.

*#KAZIINAONGEA*

Post a Comment

0 Comments